Wadau wa Sekta ya Maziwa Watakiwa Kupunguza Bei ili Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni Ufanikiwe

 Na Mwandishi Wetu,  Mwanza 


SERIKALI imewataka wadau wa sekta ya uchakataji wa maziwa Jijini Mwanza kuangalia uwezekano wa kupunguza bei ya bidhaa hiyo muhimu ili kurahisisha uendeshaji wa mpango wa maziwa mashuleni. 
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti ametoa wito huo jana Jijini mwanza katika hotuba yake wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Unywaji Maziwa Shuleni Duniani ambapo Kitaifa yalifanyika mkoani humo. 

Amewataka wadau (viwanda) wanaohusika na uchakataji na usindikaji wa maziwa Jijini humo kuangalia uwezekano wa kupunguza bei, iwe angalau Sh1,800 kwa nusu lita, kwa maziwa yaliyochakatwa na kuongezewa thamani (virutubisho muhimu).

Waziri Mnyeti amesema Serikali imefuta tozo zote zinazohusu maziwa hivyo ni busara na vyema kwa mamlaka husika kuangalia namna ya kupunguza bei za vifungashio ili kuwawezesha wachakataji wa bidhaa za maziwa kuweza kupunguza bei pia.

"Bado Mkoa kama wa Mwanza unakabiliwa na hali ya udumavu wa watoto hali ambayo kwa kiasi kikubwa imechangiwa na ukosefu wa lishe bora, hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha unywaji wa maziwa uwe sehemu ya mlo wa mtoto shuleni." amesisitiza Mhe.Mnyeti. 

Amesema itakuwa ni kazi bure kuendelea kuhimiza unywaji wa maziwa kila ifikapo kilele cha maadhimisho hayo wakati wazazo wengi wanashindwa kumudu gharama ya kuwanunulia bidhaa hiyo watoto wao.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi ameishukuru Wizara kwa kuona umuhimu wa maadhimisho hayo kufanyika Mkoani humo kutokana na miradi mingi ya kuboresha mifugo inatekelezwa mkoani Mwanza,  ikiwa ni pamoja na mradi wa Shamba la Taifa la Mifugo Mabuki na kwenye baadhi ya wilaya.

"Mhe. mgeni rasmi Serikali ya awamu ya sita imeleta mitamba 500 Mkoani Mwanza kwa ajili ya kuleta tija ya maziwa na nyama kwa wafugaji, pia wapo vijana wanaopatiwa mafunzo maalum ya ufugaji wa kisasa huko Mabuki," alieleza. 

Kwa upande wake, Msajili wa Bodi ya Maziwa, Dkt. George Msalya,  amesema sekta ya maziwa nchini Tanzania bado inakabiliwa na changamoto kadhaa.

"Bado tuna changamoto ya unywaji wa maziwa nchini ambapo hadi sasa mtu mmoja anakunywa lita 62 kwa mwaka wakati kwa mujibu wa mwongozo wa Shirika la Afya la  kimataifa mtu mmoja anatakiwa kunywa lita 200 kwa mwaka, hivyo inahitajika kazi ya ziada kuhamasisha jamii umuhimu wa kunywa maziwa," Dkt. Msalya alieleza. 

Kuelekea kilele hicho Bodi ya Maziwa ilifanya zoezi la ugawaji wa maziwa shuleni na utoaji wa elimu kwa baadhi ya shule Mkoani Mwanza pamoja na kufanya kongamano lililowahusisha wadau wa Tasnia ya Maziwa na walimu.

Kila Jumatano ya mwisho wa Septemba Tanzania inajumuika na Mataifa mengine ulimwenguni kuadhimisha siku ya unywaji maziwa shuleni ambapo kauli mbiu ya mwaka huu inasema "Mpe mtoto maziwa kwa maendeleo bora Shuleni".



Post a Comment

Previous Post Next Post