Mradi wa Tuinuke Pamoja, unaotekelezwa na Aga Khan Foundation kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania, umeendelea kuwa chachu ya kuwawezesha wanawake na kuchangia katika usawa wa kijinsi kupitia Nyanja ya kichumi na kijamii; mafunzo, ujasiriamali na ushiriki katika maonesho ya biashara.
Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Afisa Mradi wa Tuinuke Pamoja, Nahumu Fungo, alisema mradi huo wa miaka mitatu kwa sasa unatekelezwa katika halmashauri sita za Mkoa wa Dodoma ambazo ni Dodoma Jiji, Chamwino, Bahi, Chemba, Kondoa DC na Kondoa TC.
Alisema lengo kuu la mradi ni kuwawezesha vikundi vya kijamii kuwa na sauti ya Pamoja katika kuleta usawa wa kijinsia na Kuwawezesha wanawake kwa kusaidia kuendeleza jitihada zao kama vikundi katika kuleta usawa wa kijinsia ikiwemo, kujenga uwezo wa kiuchumi na kuwaimarisha katika shughuli mbalimbali za uzalishaji na biashara. Aidha, matarajio ya mradi ni kuhakikisha Wilaya za Mpwapwa na Kongwa pia zinafikiwa kabla ya mradi kukamilika.
Fungo alisema mradi umekuwa ukiwakutanisha wanawake katika majukwaa mbalimbali ya kijinsia na kiuchumi ili wapate nafasi ya kujifunza kutoka kwa wenzao, kubadilishana uzoefu na kuona mbinu bora za uzalishaji na uendeshaji wa biashara na harakati za vuguvugu la kuhakikisha jamii ya Dodoma na Tanzania inajengwa katika usawa wa kijinsia.
Katika maonesho ya Sabasaba, mradi umefanikisha kushirikisha vikundi 10 vya wanawake kati ya vikundi vingi vinavyonufaika na mradi huo. Ushiriki huo unalenga kuwapa fursa ya kuonesha bidhaa zao, kujifunza namna wafanyabiashara wengine wanavyoendesha shughuli zao na kupata masoko mapya.
“Tunatarajia wanavikundi hawa watatoka hapa na maarifa mapya watakayoyatumia kuboresha biashara zao. Pia tunawaunganisha na wadau mbalimbali wa masoko ili wajifunze zaidi na kubadilishana mawasiliano kwa ajili ya fursa za baadaye,” alisema Fungo.
Aliongeza kuwa maonesho hayo yanawapa wanawake wa vijijini nafasi ya kujionea teknolojia mbalimbali ambazo kwa kawaida huwa ni vigumu kuzipata katika mazingira yao. Kupitia teknolojia hizo, wataweza kuongeza ubora wa uzalishaji na thamani ya bidhaa zao.
Kwa mujibu wa Fungo, mradi pia umekuwa ukiwaunganisha wanufaika na taasisi mbalimbali kama SIDO zinazotoa mafunzo ya ujasiriamali na uzalishaji. Vilevile, wamekutana na wadau wengine kama Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC), pamoja na kampuni zinazojihusisha na kuongeza thamani ya bidhaa, hatua inayotarajiwa kuwasaidia wanawake kuboresha biashara zao.
Alisema ushiriki katika Sabasaba ni mwanzo wa safari ya mafanikio kwa wanavikundi hao, ambao wanatarajiwa kuwa mabalozi wa kuwafundisha wenzao walichojifunza na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika jamii zao.
Aidha, aliwahimiza kuongeza uzalishaji wa bidhaa zao na kuendelea kutumia kila fursa ya mafunzo inayojitokeza, ikiwemo Maonesho ya Nanenane, kwa kuwa si vikundi vyote vilivyopata nafasi ya kushiriki Sabasaba mwaka huu.
Pia aliwataka wanavikundi waliopata nafasi ya kushiriki maonesho hayo kutumia muda wao kujifunza kutoka kwa wafanyabiashara wengine, kubadilishana uzoefu na mawasiliano, pamoja na kutafuta mbinu mpya za kuongeza thamani na mauzo ya bidhaa zao.
WANUFAIKA WASEKA MAISHA YAMEBADILIKA.
Mmoja wa wanufaika wa mradi huo, Shamira Ibrahim Athumani kutoka kikundi cha Kondoa Women Group, alisema ushiriki wao katika Sabasaba umewapa nafasi ya kujifunza zaidi na kupata masoko ya uhakika.
Kikundi hicho kinajishughulisha na utengenezaji wa sabuni za maji, sabuni za mche, shampoo, batiki pamoja na ufugaji wa kuku.
Shamira alisema kabla ya kupata mafunzo na uwezeshwaji kutoka mradi wa Tuinuke Pamoja, walikuwa wakizalisha bidhaa kwa kiwango cha chini na zenye ubora usioridhisha. Hata hivyo, kupitia mafunzo ya biashara, usindikaji, ufugaji wa kuku na elimu kuhusu ukatili wa kijinsia, sasa wana uwezo wa kuzalisha bidhaa zenye ubora na zinazokidhi mahitaji ya soko.
Aliwashukuru wafadhili wa mradi huo kwa kuwawezesha wanawake kutoka katika hali duni ya kiuchumi hadi kufikia hatua ya kujipatia kipato cha kuendesha familia zao.
“Mradi huu umetujengea uwezo wa kujiamini na kufanya biashara kwa ufanisi. Tunaamini hata baada ya mradi kuisha, kila mmoja wetu ataweza kujitegemea na hata kuanzisha biashara binafsi kutokana na maarifa tuliyopata,” alisema Shamira.
Kwa upande wake, Peter Alocye Msambazi kutoka kikundi cha Mafanikio Hub cha Wilaya ya Chemba alisema mradi huo umewapa fursa nyingi ikiwemo kushiriki Sabasaba, kujifunza mbinu bora za uzalishaji na kuuza bidhaa zao.
Alisema kupitia mafunzo hayo wameongeza uelewa wa kuzalisha bidhaa bora zaidi na pia wameelimishwa kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, jambo ambalo limekuwa na mchango mkubwa katika jamii zao.
Naye Mwenyekiti wa kikundi cha Girls Power kutoka Wilaya ya Chamwino, Esther Kapurwa, alisema kikundi chao kinazalisha sabuni kwa matumizi ya majumbani na maofisini na pia wanatengeneza batiki zenye ubora kupitia mafunzo waliyopata SIDO katika mradi huu.
Aliwashukuru Aga Khan Foundation pamoja na Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania kwa kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia Mradi wa Tuinuke Pamoja.
Kwa mujibu wake, ushiriki katika maonesho ya Sabasaba utawajengea uwezo wa kupanua biashara zao, kuboresha bidhaa wanazozalisha na kuwahamasisha mabinti pamoja na watu wenye ulemavu kujiunga katika shughuli za uzalishaji na ujasiriamali.
Alisema matarajio yao ni kuendelea kuboresha bidhaa zao ili ziweze kushindana katika soko la ndani na nje ya nchi, huku wakiendelea kuwa mfano wa wanawake wanaoweza kujiletea maendeleo kupitia elimu, ubunifu na ujasiriamali.




Post a Comment