Na Edward Winchislaus.
Sanaa ya uchoraji wa nyumba za tembe iliyowahi kuwa sehemu ya utambulisho wa jamii ya Wagogo na ambayo kwa miaka mingi imeendelea kutoweka kutokana na mabadiliko ya maisha na makazi, sasa imeanza kupata uhai mpya baada ya kuzinduliwa kwa mradi wa Mama Tembe, unaolenga kuokoa urithi huo wa kiutamaduni huku ukiwawezesha wanawake na wasichana kujenga uchumi kupitia ubunifu wa asili.
Mradi huo unaotekelezwa na Shirika la Innovation Development for Future Generation (IDFG) kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uswisi na Norway kupitia programu ya Articipesezi, utadumu kwa miezi sita na unawahusisha wanawake wazee 15 wa kabila la Kigogo watakaowarithisha mabinti 20 pamoja na wanafunzi kutoka shule tatu mbinu za uchoraji wa jadi kwa kutumia zana na malighafi za asili zilizokuwa zikitumiwa kupamba nyumba za tembe.
Akizindua mradi huo Julai 9,2026 kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Kaimu Mkurugenzi Dkt. Sophia Nchimbi alisema hatua hiyo inaunga mkono juhudi za serikali za kuhifadhi urithi wa taifa huku ikifungua fursa mpya za maendeleo kupitia utamaduni.
Alisema uchoraji wa nyumba za tembe si mapambo ya kawaida, bali ni sehemu ya historia ya Wagogo inayobeba utambulisho wa jamii hiyo, hivyo kurejeshwa kwake kutasaidia kuitangaza Chamwino kama kitovu cha utalii wa utamaduni na kuongeza thamani ya kazi za ubunifu zinazofanywa na wananchi.
"Tunafungua ukurasa mpya wa kuhifadhi utamaduni wetu. Kupitia mradi huu, Chamwino itanufaika kwa kuitangaza historia na utamaduni wake, lakini pia wananchi watanufaika kiuchumi kupitia kazi za sanaa. Kama Halmashauri tutaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha mradi huu unafanikiwa," alisema Dkt. Nchimbi.
Aidha, aliwataka wanawake na mabinti watakaopata mafunzo hayo kuyatumia kama mtaji wa maisha yao, badala ya kuyaona kama shughuli ya muda mfupi, ili ujuzi watakaoupata uweze kuwanufaisha hata baada ya mradi kukamilika.
Kwa upande wake, Afisa Utamaduni wa Wilaya ya Chamwino, Bw.Jackson Kitija, alisema mradi huo umefika katika kipindi muhimu ambapo baadhi ya maarifa ya jadi yalikuwa yameanza kupotea kutokana na wazee waliokuwa nayo kuendelea kuzeeka huku vijana wengi wakikosa nafasi ya kujifunza.
Alisema uchoraji wa nyumba za tembe ni sehemu ya urithi usiogusika wa taifa na kwamba kuwarithisha vijana maarifa hayo ni njia sahihi ya kuhakikisha historia na utamaduni wa Wagogo vinaendelea kuishi.
Naye,Mkurugenzi wa Innovation Development for Future Generation (IDFG),Bi. Victoria Mponda, alisema mradi wa Mama Tembe umeandaliwa baada ya utafiti kubaini kuwa wanawake wa Kigogo walikuwa na mchango mkubwa katika kuhifadhi utamaduni kupitia michoro waliyoifanya kwenye nyumba za tembe, lakini mchango huo haukuwa umetambuliwa wala kuhifadhiwa kwa kiwango kinachostahili.
Alisema zamani wanaume walikuwa wakijenga nyumba huku wanawake wakizipamba kwa michoro iliyobeba alama na maana mbalimbali za maisha ya jamii. Hata hivyo, kutokana na kupungua kwa nyumba za tembe, ujuzi huo ulianza kupotea na wengi wakabaki kuujua kupitia simulizi za wazee.
Kwa mujibu wa Mponda, mradi huo hautaishia kutoa mafunzo pekee, bali utafanya kazi ya kukusanya historia ya michoro hiyo, kueleza maana ya kila mchoro na kuhifadhi taarifa zote kwa mfumo wa kidigitali ili ziwe rejea kwa vizazi vijavyo.
Alisema hatua nyingine ni kuhakikisha ubunifu wa wanawake hao unalindwa kwa kupata hati miliki, huku michoro hiyo ikitumika kutengeneza bidhaa mbalimbali zenye thamani ya kiuchumi ikiwemo mavazi yatakayobeba utambulisho wa sanaa ya Wagogo.
"Tunataka wanawake hawa watambulike kama wabunifu wa sanaa hii. Tutahifadhi kazi zao kidigitali, tutazisajili kwa hati miliki na baadaye kuzibadili kuwa bidhaa zitakazoweza kuuzwa. Hii itasaidia kulinda urithi wetu lakini pia kuwapa wanawake fursa ya kujipatia kipato kutokana na ubunifu wao," alisema Mponda.
Alisema moja ya changamoto kubwa waliyoikabili wakati wa kuanza mradi huo ilikuwa kuwashawishi wanawake wazee kushiriki, kwa kuwa wengi walikuwa hawaamini kuwa uchoraji walioutumia kwa miaka mingi kupamba nyumba unaweza kuwa shughuli yenye faida ya kiuchumi.
"Kwa kushirikiana na viongozi wa serikali na wa kimila tuliwafikia na kuwajengea uelewa kuwa sanaa nayo ni uchumi. Leo wamekubali kurithisha maarifa yao kwa mabinti, jambo ambalo tunaamini litakuwa mwanzo wa kufufua sanaa iliyokuwa ikielekea kutoweka," alisema.
Miongoni mwa wanufaika wa mradi huo ni Bi.Esteli Chibaya (84), mkazi wa Chamwino, ambaye alisema amefurahishwa na hatua ya kupewa nafasi ya kurithisha ujuzi alioupata tangu akiwa msichana, akiamini kuwa vijana wataendelea kuuenzi utamaduni wa Wagogo badala ya kuuacha upotee.
"Tulikuwa tunachora nyumba kwa ajili ya kuzipamba bila kujua kuwa siku moja ujuzi huu ungekuwa sehemu ya maendeleo yetu. Leo nina furaha kuona watoto na wajukuu wetu wataurithi na kuutumia kujenga maisha yao," alisema Chibaya.
Mradi wa Mama Tembe unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu, huku wadau wakiamini kuwa mbali na kurejesha sanaa ya uchoraji wa nyumba za tembe, utafungua ukurasa mpya wa kuhifadhi urithi wa Wagogo, kuimarisha utalii wa utamaduni na kuwapa wanawake nafasi ya kutumia maarifa ya jadi kama nyenzo ya kujiletea maendeleo.












Post a Comment