‎WIZARA YA MAMBO YA NDANI YAOMBA BAJETI YA TRILIONI 2.4 KWA MWAKA 2026/2027

 

Na Edward Winchislaus

‎Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Paschal Katambi Patrobass (Mb), leo Mei 25, 2026 amewasilisha hotuba ya bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/2027 na kuliomba Bunge kuidhinisha jumla ya Shilingi trilioni 2.44 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara hiyo katika mwaka mpya wa fedha.


‎Amesema kati ya fedha hizo, Shilingi trilioni 1.95 sawa na asilimia 80 ya bajeti yote zimetengwa kwa matumizi ya kawaida. Kati ya fedha hizo, Shilingi trilioni 1.18 zimeelekezwa kwenye mishahara ya watumishi huku Shilingi bilioni 769.5 zikitarajiwa kutumika kwa matumizi mengineyo ya Wizara na taasisi zake.


‎Aidha, Waziri Katambi amesema Shilingi bilioni 489.8 sawa na asilimia 20 ya bajeti yote zimepangwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Amefafanua kuwa Shilingi bilioni 453.9 ni fedha za ndani huku Shilingi bilioni 35.8 zikiwa ni fedha za nje zitakazosaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya Wizara hiyo.


‎Katika hatua nyingine, Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi limeendelea kuimarisha uwezo wake wa kiuchumi baada ya kukusanya mapato ghafi ya Shilingi bilioni 7.66 katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, ikilinganishwa na Shilingi bilioni 3.4 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.


‎Waziri Katambi amesema Shirika hilo limeendelea kuendesha miradi mbalimbali ya kibiashara ikiwemo huduma za usalama kwa taasisi binafsi na za umma, usafirishaji wa fedha za benki, ushonaji wa sare pamoja na huduma katika Bandari ya Dar es Salaam. Aidha, amesema Shirika limesaini mkataba mpya na NMB Bank wa kuongeza huduma za usindikizaji wa fedha katika mashine za ATM sambamba na ununuzi wa magari maalum ya kusafirishia fedha ili kuongeza ufanisi wa huduma hiyo.

Post a Comment

Previous Post Next Post