Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa ameliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya Shilingi trilioni 1.8 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za Wizara ya Afya katika mwaka wa fedha 2026/27 .
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi Bungeni jijini Dodoma Mei 11, 2026, Mhe. Mchengerwa amesema kati ya fedha hizo, Shilingi trilioni 1.148 sawa na asilimia 64 ya bajeti yote zitatumika katika miradi ya maendeleo ya sekta ya afya nchini.
Amefafanua kuwa kati ya fedha za maendeleo, Shilingi bilioni 789.45 ni fedha za ndani huku Shilingi bilioni 358.56 zikitarajiwa kutoka kwa washirika wa maendeleo kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya afya.
Kwa upande wa matumizi ya kawaida, Waziri huyo amesema Wizara imepanga kutumia Shilingi bilioni 652.236 sawa na asilimia 36 ya bajeti yote, ambapo Shilingi bilioni 516.323 zitatumika kulipa mishahara ya watumishi wa afya na Shilingi bilioni 135.913 kwa matumizi mengineyo.
Mhe. Mchengerwa amesema serikali ya awamu ya sita imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, nafuu na zenye staha katika maeneo yote ya nchi.Katika bajeti hiyo, Serikali imeweka vipaumbele 11 vitakavyoiongoza Wizara ya Afya mwaka 2026/27 kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za afya na kuifanya Tanzania kuwa mfano barani Afrika.
Moja ya maeneo yatakayopata msukumo mkubwa ni utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, ambapo Serikali itaendelea kusajili kaya zenye uhitaji na kuhamasisha wananchi wengi zaidi kujiunga na mfumo huo wa huduma za afya.
Aidha, Serikali imepanga kuongeza uwekezaji katika viwanda vya ndani vya dawa na bidhaa za afya ili kuhakikisha upatikanaji wa dawa muhimu unaimarika sambamba na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Waziri Mchengerwa amesema Serikali pia itaendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika hospitali na vituo vya afya kwa kuunganisha mifumo ya taarifa za afya, kuongeza huduma za afya kwa njia ya mtandao pamoja na matumizi ya akili unde katika utoaji wa huduma.
Katika hatua nyingine, Serikali imetangaza mpango wa kuajiri wahudumu wa afya ngazi ya jamii 8,000 katika mwaka ujao wa fedha, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi mijini na vijijini pamoja na kuimarisha mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko na yasiyoambukiza.


Post a Comment