Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha sekta ya elimu nchini ikiwemo kufanya mapitio ya sheria ya elimu ili kuendana na utekelezaji wa sera mpya ya elimu na mafunzo ya mwaka 2023.
Akizungumza leo Mei 21, 2026 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa kikao cha wadau wa elimu kujadili mapitio ya Sheria ya Elimu, Waziri Mkenda amesema mageuzi ya elimu hayaishii kwenye sera na mitaala pekee bali yanahusisha maeneo mengi muhimu yanayolenga kuongeza ubora wa elimu nchini.
Amesema Serikali imekuwa ikizingatia maeneo saba muhimu katika mageuzi hayo ambayo ni sera, sheria, mitaala, idadi ya walimu na wakufunzi, ubora wa walimu na wakufunzi pamoja na miundombinu na vitendea kazi vya kufundishia na kujifunzia.
Aidha amesema Serikali imeendelea kujenga miundombinu ya elimu kuanzia shule za awali hadi vyuo vikuu pamoja na kampasi mbalimbali nchini huku ikiendelea kuboresha upatikanaji wa vitendea kazi ikiwemo vitabu na vifaa vya kujifunzia.
“Nchi yetu sasa imefikia hatua ambayo utekelezaji wa sera mpya unahitaji uelekeo wa kisheria kwani elimu ya lazima imeongezwa kutoka miaka saba hadi miaka 10 mpaka kidato cha nne, hivyo sheria lazima ibadilishwe ili iakisi mabadiliko hayo na kutupa nyenzo ya kutekeleza sera yetu,” amesema Profesa Mkenda.
Waziri huyo amesema sheria ya elimu iliyopo ilitungwa mwaka 1978 na imefanyiwa marekebisho mbalimbali, hivyo maoni yatakayokusanywa kutoka kwa wadau yatachakatwa na kuwasilishwa Serikalini ili kuamua kama kutafanyika marekebisho ya sheria iliyopo au kutungwa sheria mpya kabisa ya elimu.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Mhe.Wanu Hafidh Ameir amesema lengo la kikao hicho ni kusikiliza taarifa ya awali ya mapitio ya Sheria ya Elimu Sura ya 353 iliyotayarishwa baada ya ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wa sekta ya elimu nchini.
Amesema mchakato huo ulioanza mwaka 2024 umechukua muda mrefu ili kuhakikisha makundi yote ya wadau yanapata uwakilishi wa kutoa maoni yatakayosaidia kupatikana kwa sheria bora itakayodumu kwa vizazi vingi vijavyo huku akiwataka washiriki kuweka mbele maslahi ya taifa wakati wa mijadala hiyo.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Carolyne Nombo amesema Wizara imejipanga kuyachakata na kuyafanyia kazi maoni yote yatakayotolewa na wadau ili kuboresha taarifa ya mwisho itakayowasilishwa Serikalini kwa ajili ya maamuzi kuhusu mustakabali wa sheria mpya ya elimu nchini.






Post a Comment