‎SERIKALI YAWAPA MOTISHA WATAHINIWA: UFADHILI WA NDANI NA NJE KUWASUBIRI WATAKAOFANYA VIZURI ‎

 

‎Na Edward Winchislaus.

‎Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Mhe.Prof. Adolf Mkenda, amesema serikali imeendelea kuweka mkazo kwenye motisha na fursa za elimu kwa watahiniwa wa kidato cha sita na vyuo vya ualimu, huku akisisitiza kuwa mafanikio yao yatafungua milango ya ufadhili wa masomo ndani na nje ya nchi.

‎Akizungumza leo Mei 4, 2026 katika viwanja vya Bunge, Waziri Mkenda amesema jumla ya wanafunzi 133,655 wa kidato cha sita wameanza mitihani yao, huku walimu 14,679 nao wakiwa wameanza mitihani yao ya kuhitimu mafunzo rasmi ya ualimu.

‎Amesema hadi sasa mwenendo wa mitihani hiyo umekuwa mzuri na wa utulivu, huku serikali ikiwa imeendelea kuimarisha usimamizi ili kuhakikisha haki na uwazi vinatawala katika mchakato mzima wa upimaji.

‎“Hatupendi kupoteza mtu yeyote katika mitihani hii, lakini yeyote atakayekiuka kanuni tutamchukulia hatua,” amesema Waziri Mkenda, akionya dhidi ya udanganyifu.

‎Katika kuhamasisha ufaulu bora, amesema serikali imeendelea kutoa fursa mbalimbali kwa wanafunzi wanaofanya vizuri, ikiwemo kujiunga na vyuo vikuu na kupata mikopo kulingana na ufaulu wao pamoja na hali za kifamilia.

‎Amefafanua kuwa kupitia mpango wa Samia Scholarship, wanafunzi bora wa masomo ya sayansi wamekuwa wakifadhiliwa kwa asilimia 100 kusoma katika vyuo vya ndani, hasa katika fani za kimkakati kama uhandisi, tiba, TEHAMA na sayansi asilia.

‎Aidha, amesema serikali imeanzisha na kuendeleza mpango wa Samia Scholarship Extended unaolenga kuwainua zaidi wanafunzi 50 bora, hasa wa masomo yenye hisabati, kwa kuwapatia mafunzo maalum kabla ya kupelekwa nje ya nchi kusoma taaluma za kisasa kama akili unde (AI) na sayansi ya data.

‎Kwa mujibu wa Waziri Mkenda, tayari wanafunzi 16 wamekwenda kusoma katika Chuo Kikuu cha Johannesburg nchini Afrika Kusini, huku wengine 34 wakiwa wamepelekwa Ireland, 32 katika Chuo Kikuu cha Limerick, na wawili katika chuo cha USD nchini humo kusomea shahada ya kwanza katika taaluma za akili unde.


‎Katika hatua nyingine, walimu walionufaika na mafunzo ya nje ya nchi wameeleza uzoefu wao, akiwemo Jackline Juliasi aliyepata mafunzo nchini India katika Chuo Kikuu cha Sharda, akisema wamejifunza matumizi ya teknolojia za kisasa za ufundishaji na tathmini za kidigitali.

‎Kwa upande wake, mwalimu Sungura Durunga amesema mafunzo hayo yamewafungua zaidi kuhusu umuhimu wa kuoanisha elimu na mahitaji halisi ya dunia, akisisitiza haja ya kuimarisha masomo ya teknolojia kama akili unde ili kuwajenga vijana wanaokwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.


Post a Comment

Previous Post Next Post