Wakati serikali ikiendelea kuimarisha sekta za uzalishaji nchini, vijana wameendelea kupata fursa zaidi za kujiajiri kupitia uwekezaji katika shughuli za uvuvi na mifugo.
Hali hiyo imekuja baada ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt.Bashiru Ally Kakurwa kuliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya Shilingi bilioni 476.6 kwa mwaka wa fedha 2026/27 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za wizara hiyo.
Akiwasilisha bajeti hiyo jijini Dodoma Mei 14, 2026, Waziri Bashiru amesema kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 101.5 zimeelekezwa kwenye matumizi ya kawaida huku Shilingi bilioni 375.1 zikitengwa kwa miradi ya maendeleo.
Amesema serikali imeendelea kuweka mkazo katika kuongeza uzalishaji wa mifugo na mazao ya uvuvi sambamba na kuimarisha masoko na kudhibiti magonjwa ya mifugo nchini.
Katika hatua nyingine, amesema serikali imetoa Shilingi bilioni 7 zilizowawezesha vijana 308 kuwekeza katika miradi mbalimbali ya uchumi wa buluu kupitia sekta ya uvuvi.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, vijana hao wamejikita katika ufugaji wa samaki kwenye vizimba, kilimo cha mwani, ufugaji wa majongoo bahari pamoja na unenepeshaji wa kaa kwa lengo la kuongeza kipato na ajira.
Aidha, serikali imeendelea kupambana na uvuvi haramu ambapo operesheni mbalimbali zimefanikisha kukamatwa kwa nyavu haramu, kokoro, boti na injini zilizokuwa zikitumika kinyume cha sheria.
Bashiru amesema jumla ya watuhumiwa 1,047 wamekamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria huku elimu ya uvuvi endelevu ikiendelea kutolewa kwa jamii za wavuvi katika mikoa mbalimbali nchini.
Katika sekta ya mifugo, amesema uzalishaji wa maziwa umeongezeka kwa asilimia 5.2 na kufikia lita bilioni 4.2 mwezi Aprili 2026 kutokana na kuongezeka kwa ng’ombe bora wa maziwa na utoaji wa elimu ya ufugaji wa kisasa kwa wafugaji.


Post a Comment