‎TESP YAINUA WALIMU NA UBORA WA ELIMU TANZANIA ‎

 


Na Edward Winchislaus

‎Serikali ya Tanzania imeendelea kuimarisha sekta ya ualimu kupitia Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu (TESP), uliotekelezwa kwa ushirikiano na Serikali ya Canada kupitia Global Affairs Canada (GAC), ukiwa na lengo la kuboresha ubora wa walimu na elimu kwa ujumla.

‎Akizungumza Aprili 9, 2026 jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema mradi huo umechangia kwa kiasi kikubwa mageuzi ya maandalizi ya walimu, akisisitiza kuwa ubora wa walimu una nafasi muhimu katika kuinua kiwango cha elimu nchini.

‎Amebainisha kuwa Serikali imewekeza takribani shilingi bilioni 140, huku Global Affairs Canada ikichangia bilioni 92, fedha zilizotumika kuboresha miundombinu, vifaa vya kufundishia na mifumo ya TEHAMA katika vyuo 34 vya ualimu.

‎Kupitia uwekezaji huo, vyuo vimejengewa maabara, maktaba na kuongezewa vitabu, sambamba na kuunganishwa kwenye mfumo wa maktaba wa pamoja (COTUL) unaorahisisha upatikanaji wa rasilimali za kielimu.

‎Aidha, vyuo 25 vya ualimu vimeunganishwa na Mkongo wa Taifa, hatua iliyowezesha matumizi ya teknolojia za kidijitali katika ufundishaji na ujifunzaji, na hivyo kuongeza ufanisi katika utoaji wa mafunzo.

‎Mradi huo pia umezingatia masuala ya ujumuishi na usawa wa kijinsia, kwa kuhakikisha fursa sawa zinapatikana kwa walimu na wanafunzi wote katika mafunzo na uongozi.

‎Katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, TESP imewezesha ujenzi wa miundombinu rafiki kwa mazingira, ikiwemo matumizi ya nishati mbadala kama jua na biogas, hatua iliyopunguza gharama za uendeshaji kwa kiasi kikubwa.

‎Kwa upande wa wadau, Mkuu wa Chuo cha Ualimu Tabora, Bi. Balbina Joseph, amesema mradi huo umeongeza ufanisi wa wakufunzi na watumishi kupitia mafunzo ya uongozi na usimamizi, pamoja na kuboresha mazingira ya kazi.

‎Naye mwanafunzi Marry Faustine Igulu kutoka Chuo cha Ualimu Bustani amesema maboresho ya miundombinu, maabara na vifaa vya TEHAMA yameimarisha mazingira ya kujifunzia, huku Serikali ikiahidi kuendeleza mafanikio ya TESP hata baada ya ushirikiano na wadau kukamilika.

Post a Comment

Previous Post Next Post