Serikali imesema katika mwaka fedha wa 2026/27, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma itatekeleza vipaumbele vikuu viwili (2) ikiwa ni pamoka na kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma kwa Taasisi na kwa wananchi ili kuweza kuwafikia kwa urahisi.
Hayo yamebainishwa leo Aprili 17,2026 Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete wakati akiwasilisha bajeti ya ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Mbali na kipaumbele hicho amesema kingine ni kuendelea kuwaelimisha viongozi wa umma kuhusu kuimarisha uwajibikaji wa pamoja miongoni mwa viongozi wa umma hususani katika ngazi ya halmashauri (wakuu wa idara na madiwani).
"Katika mwaka 2026/27, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imepanga kutekeleza shughuli zifuatazo, Kupokea na kuhakiki Matamko ya Rasilimali na Madeni kwa Viongozi waUmma kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Sura 398, Kuchunguza tuhuma za uvunjifu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Sura 398,Kupokea malalamiko na taarifa za ukiukwaji wa maadili kwa mujibu wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma kutoka kwa wananchi,"amesema.
Ameongeza kuwa itakamilisha ujenzi wa Ofisi Kanda ya Ziwa (Mwanza) na kuendelea na ujenzi wa Ofisi za Nyanda za Juu Kusini (Mbeya) na Mashariki (Morogoro) pamoja na kuanza kwa ujenzi wa Jengo la Kanda ya Kaskazini (Arusha).
Katika mwaka 2026/27, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imeomba kuidhinishiwa shilingi Bilioni 18.07 kwa ajili ya kutekeleza kazi zilizopangwa.
"Kati ya fedha hizo, shilingi Bilioni 15 sawa na asilimia 83.40 kwa ajili ya Matumizi ya kawaida,na shilingi Bilioni 3 sawa na asilimia 16.60 kwa ajili ya Matumizi ya Miradi ya Maendeleo,"amesema.

Post a Comment