Na Edward Winchislaus
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, amesema serikali inaendelea kuchukua hatua za haraka kushughulikia malalamiko ya wananchi kupitia programu ya 'Sema na Waziri' inayowapa fursa ya kuwasilisha changamoto zao moja kwa moja.
Akitoa mrejesho wa programu zilizopita leo Aprili 22,2026 jijini Dodoma Dkt. Homera ameeleza kuwa programu hiyo imekuwa daraja muhimu kati ya wananchi na serikali katika kutatua migogoro mbalimbali ya kijamii na kisheria.
Amesema tangu kuanzishwa kwa programu hiyo Machi 17 mwaka huu, jumla ya malalamiko 2,277 yamepokelewa na kufanyiwa kazi, huku wastani wa malalamiko 67 yakipokelewa kwa kila kipindi. “Programu hii inaendelea kuwa chombo madhubuti cha kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi popote walipo nchini,” amesema.
Miongoni mwa kesi zilizopokelewa ni ya mwanafunzi Salma Omari kutoka chuo cha DIT Kampasi ya Mwanza, aliyekumbwa na mkanganyiko wa kozi uliomfanya kushindwa kuona matokeo yake. Wizara imeeleza kuwa tayari imewasiliana na uongozi wa chuo husika ili kuhakikisha mwanafunzi huyo anapatiwa haki yake ya kusoma kozi anayoihitaji bila kupoteza muda zaidi.
Katika tukio lingine, Joyce Samson kutoka Mvomelo aliripotiwa kukumbwa na tuhuma za utekaji baada ya kumsaidia mtoto aliyepotea, hali iliyosababisha vitisho na unyanyasaji. Dkt. Homera amesema wizara imeunda timu ya wataalamu kufuatilia suala hilo na pia imehusisha wataalamu wa sheria kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe ili kuhakikisha haki inapatikana kwa haraka.
Aidha, malalamiko ya fidia ya ardhi kutoka kwa Rahim Mussa Ngema wa Mtwara yameanza kushughulikiwa, ambapo wizara imewasiliana na Wizara ya Ardhi kupitia barua rasmi ya Aprili 20, 2026 ili kupata ufafanuzi wa kina na kuharakisha suluhisho la mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu.
Kwa upande wa ukatili wa kijinsia, wizara imepongeza Jeshi la Polisi kwa kuchukua hatua za haraka katika tukio la Simiyu lililohusisha mama aliyekuwa akipigwa na mumewe. Mtuhumiwa tayari amekamatwa na anaendelea kuhojiwa kabla ya kufikishwa mahakamani.
Akizungumzia mwenendo wa malalamiko, Dkt. Homera amesema migogoro ya ardhi inaongoza kwa asilimia 31.3, ikifuatiwa na ajira (19.4%) na madai (13.4%), huku masuala mengine yakijumuisha mirathi, msaada wa kisheria na ukatili wa kijinsia. Kati ya malalamiko yote, asilimia 56.7 tayari yamepatiwa ufumbuzi.
“Tunawahakikishia wananchi kuwa wizara imejipanga kikamilifu kushughulikia malalamiko yote kwa wakati na kwa ufanisi,” amesisitiza Dkt. Homera, akiongeza kuwa wataalamu wenye ujuzi wa kutosha wameandaliwa kushughulikia changamoto hizo.
Programu ya 'Sema na Waziri' inaendelea kurushwa mara mbili kwa mwezi, ikilenga kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususan walioko maeneo ya pembezoni, ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki na kusikilizwa.



Post a Comment