Na Edward Winchislaus
Serikali ya Tanzania imeanza hatua ya kihistoria ya kuimarisha utendaji na uwazi katika matumizi ya raslimali za umma kwa kuzindua rasmi Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari, Alex Haraba,Kaimu Kamishina wa Idara ya Fedha na Sera za Ununuzi wa Umma, amesema“Uzinduzi wa sera hii ni hatua muhimu ya kimkakati inayolenga kuimarisha usimamizi wa raslimali za umma na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za serikali.”
Uzinduzi rasmi unatarajiwa kufanyika tarehe 8 Aprili 2026 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, Jijini Dodoma, huku Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Sera hii inalenga kuweka mfumo wa kisera unaosimamia kila hatua ya mnyororo wa ugavi, kuanzia upangaji wa mahitaji, ununuzi wa umma, ugomboaji, uondoaji wa mizigo ya serikali, upokeaji na urejesheaji wa bidhaa, hadi uhifadhi wa raslimali.
Haraba amesema“Serikali inalenga kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika matumizi ya raslimali za umma pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa na huduma za ubora unaotakiwa.”
Hadi sasa, shughuli za mnyororo wa ugavi zimekuwa zikitekelezwa bila mwongozo mmoja wa kitaifa, jambo lililosababisha changamoto katika uratibu na usimamizi wa raslimali za umma.
Sera mpya inalenga kufungamanisha hatua zote za mnyororo wa ugavi, kuboresha matumizi ya raslimali, kuongeza tija na kuhakikisha kila shilingi ya umma inafika pale inapohitajika.
Aidha, Serikali inasisitiza utawala bora, matumizi ya teknolojia, ushiriki wa sekta binafsi, na kuimarisha makubaliano maalumu ya kijamii, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi na ajira kwa Watanzania.
Kupitia sera hii, Serikali inalenga kupunguza upotevu wa raslimali, kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Post a Comment