Na. mwandishi wetu,DODOMA
Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa familia, wadau na jamii kwa ujumla kutambua na kulinda haki za watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani, huku ikihimiza watendewe kwa usawa kama watoto wengine wote.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Ofisi ya Serikali ya Mtaa Nkuhungu kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto anayeishi na kufanya kazi mtaani, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, alisema ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha watoto hawa wanapata haki zao za msingi na kuishi maisha yenye staha.
Alibainisha kuwa kumekuwepo na ongezeko la watoto wa mitaani linalochangiwa na sababu mbalimbali, zikiwemo migogoro ya kifamilia na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto. Alieleza kuwa hali hiyo husababisha watoto kukimbia makazi yao na kujikuta wakiishi mitaani, jambo linalohatarisha ustawi wao.
“Kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu isemayo ‘Malezi na ulinzi wa mtoto ni jukumu letu sote’ni wazi kwamba tukishindwa kushirikiana katika malezi bora, tunachangia moja kwa moja kuongezeka kwa watoto wa mitaani” alisema Gwajima.
Alisisitiza kuwa watoto hao wanapaswa kutambuliwa, kulindwa na kupewa haki zao za msingi ikiwemo elimu, afya na malezi bora, kama ilivyo kwa watoto wengine. Aidha, aliwahimiza viongozi wa dini kushirikiana na serikali katika kutoa mafunzo ya maadili mema kwa watoto tangu wakiwa wadogo, huku akiwataka wazazi kuwa mfano bora kwa vitendo kwa watoto wao.
Dkt. Gwajima pia alielekeza kuwa juhudi zichukuliwe mapema kwa kuwapeleka watoto wenye changamoto kwenye ofisi za serikali za mitaa ili waweze kupata msaada stahiki kabla hawajaingia mitaani. Aliongeza kuwa serikali imeanzisha madawati ya jinsia na watoto katika vituo vikuu vya mabasi, ambapo hadi sasa watoto 2,969 wamehudumiwa kupitia huduma hizo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Jabiri Shekimweri, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, alisisitiza umuhimu wa kuwafundisha watoto kufanya kazi kwa misingi ya kujenga uwajibikaji, lakini akapinga vikali vitendo vya kuwatumikisha watoto kutafuta kipato kwa ajili ya familia.
“Niwito wetu kuhakikisha watoto wanafundishwa kufanya kazi kwa lengo la kuwajenga, lakini si kuwatumia kama vyanzo vya mapato ya familia. Hilo halikubaliki” alisisitiza.
Aliongeza kuwa kwa mwaka 2026, Mkoa wa Dodoma ulibaini watoto 69 waliokuwa wakiishi mitaani, ambapo juhudi za serikali zimefanikisha kuwaunganisha watoto 65 na familia zao.
Aidha, alitoa pongezi kwa maafisa ustawi wa jamii wanaofanya kazi chini ya wizara hiyo kwa mchango wao mkubwa katika kusaidia watoto wa mitaani kurejea katika mazingira salama na yenye matumaini.
changamoto ya watoto wa mitaani inaweza kudhibitiwa endapo familia, jamii, serikali na wadau mbalimbali wataungana kwa dhati kutekeleza wajibu wao. Kila mmoja ana nafasi ya kuhakikisha mtoto analelewa katika mazingira salama, yenye upendo na maadili bora. Ushirikiano huu ndio utakaokuwa suluhisho la kudumu katika kulinda kizazi cha sasa na kijacho.



Post a Comment