Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji,Mhe.Prof. Kitila Mkumbo, amewasilisha bungeni jijini Dodoma bajeti ya shilingi bilioni 144.85 kwa mwaka wa fedha 2026/27, akisisitiza kuwa inalenga kuimarisha uwekezaji na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Katika bajeti hiyo, shilingi bilioni 126.01 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida na bilioni 18.83 kwa miradi ya maendeleo, ambapo baadhi ya wabunge wameitaka Serikali kuongeza mgao wa maendeleo ili kuongeza matokeo ya moja kwa moja kwa wananchi.
Mkumbo amesema mgao huo umezingatia vipaumbele vya taifa ikiwemo kuimarisha mifumo ya uwekezaji, usimamizi wa rasilimali za umma na mipango ya maendeleo ya muda mrefu.
Kwa upande wa mafungu, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji imepangiwa bilioni 35.38, Tume ya Taifa ya Mipango bilioni 48.64, na Ofisi ya Msajili wa Hazina bilioni 60.82.
Aidha, amebainisha kuwa mtiririko wa uwekezaji kutoka nje (FDI) umeongezeka kutoka dola milioni 944 mwaka 2020 hadi dola bilioni 1.72 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 45.1.
Kwa mujibu wa ripoti ya uwekezaji ya dunia ya UNCTAD ya mwaka 2025, Tanzania imeendelea kuimarika kimtandao wa uwekezaji, ikishika nafasi ya tatu Afrika Mashariki nyuma ya Ethiopia na Uganda.
Sekta zinazoongoza kwa kuvutia uwekezaji huo ni madini, viwanda, fedha na bima pamoja na mawasiliano, zikichangia zaidi ya asilimia 80 ya uwekezaji wote nchini.

Post a Comment