DKT.HOMERA AWAPONGEZA MAWAKILI WA SERIKALI KWA UFANISI MAHAKAMANI ,AWAAHIDI OFISI ‎

 

Na Edward Winchislaus

‎Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe.Dkt.Juma Zuberi Homera, amesema serikali inawategemea kwa kiwango kikubwa mawakili wa serikali katika kuisimamia na kuishauri kwenye masuala ya kisheria yanayolenga kuharakisha maendeleo ya taifa, akisisitiza umuhimu wa taaluma hiyo katika kufikia Dira ya Maendeleo ya 2050.

‎Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) kilichofanyika Aprili 29, 2026 jijini Dodoma, Dkt.Homera amepongeza maboresho ya utendaji wa mawakili wa serikali, akibainisha kuwa kwa sasa wameongeza ufanisi mkubwa katika usimamizi wa mashauri mahakamani ukilinganisha na ilivyokuwa awali.

‎Amesisitiza haja ya mawakili hao kujifunza na kuendana na mabadiliko ya teknolojia ikiwemo akili unde (AI), pamoja na kujikita katika masuala ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) na mikataba ya rasilimali kama mafuta, gesi na madini ili kuepusha migogoro na kuisaidia serikali kufanya maamuzi sahihi ya kisheria.


‎Aidha, Dkt.Homera ameahidi kuwa serikali itaipatia TPBA ofisi ifikapo Juni 15 mwaka huu bila gharama yoyote, huku akihimiza chama hicho kujiimarisha kiuchumi kupitia mifuko ya kifedha na kueneza uongozi wake kuanzia ngazi ya wilaya hadi taifa.


‎Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe.Eliakim Maswi, amesema kikao hicho kinapaswa kuwa cha kimkakati zaidi badala ya kubaki kuwa cha taarifa, akihimiza washiriki kuweka mwelekeo mpya wa sekta ya sheria nchini.

‎Maswi ameeleza kuwa kuna umuhimu wa kujenga utambulisho wa kitaaluma wa mawakili wa serikali pamoja na kuweka msingi wa mchango wa sekta ya sheria katika safari ya taifa kuelekea Dira ya 2050, akiwataka washiriki kufikiri tofauti na kuchukua hatua za mabadiliko.

‎Hata hivyo,ameongeza kuwa taifa linaweza kuwa na rasilimali nyingi lakini bila kuwa na mfumo imara wa sheria, rasilimali hizo haziwezi kuleta matokeo chanya, hivyo kusisitiza nafasi ya sekta ya sheria kama uti wa mgongo wa maendeleo.


‎Awali, Rais wa TPBA, Bw. Bavoo Junus, amesema chama hicho kina wanachama takribani 4,600 Tanzania Bara, huku zaidi ya mawakili 1,500 wakihudhuria kikao hicho, jambo linaloonyesha ukuaji wa chama na umuhimu wake.

‎Junus alibainisha kuwa TPBA imeiomba serikali kuhakikisha mawakili wa serikali wanapatiwa ofisi za kudumu pamoja na kuwepo kwa uwiano wa mishahara kwa watumishi wa ngazi zinazofanana bila kujali wanatoka taasisi zipi, ili kuongeza motisha na ufanisi kazini.

Post a Comment

Previous Post Next Post