‎SERIKALI YASISITIZA USHIRIKIANO WA WADAU KUBORESHA LISHE NA HUDUMA MUHIMU SHULENI ‎

 


‎Na Edward Winchislaus.

‎Serikali imetoa wito kwa wadau wa elimu, lishe na maendeleo kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula bora, maji safi na huduma muhimu shuleni kwa lengo la kuboresha afya na mazingira ya kujifunzia.

‎Akizungumza jijini Dodoma leo Machi 12.2026 katika maadhimisho ya Siku ya Utoaji wa Chakula Shuleni Afrika 2026, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidhi Ameir, amesema suala la lishe shuleni linahitaji ushiriki wa sekta mbalimbali kwa kuwa ni jukumu la pamoja la serikali, wazazi na wadau wengine.

‎Amesema serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuhakikisha huduma muhimu shuleni zinapatikana, huku akisisitiza kuwa lishe bora kwa wanafunzi ni msingi muhimu wa kuboresha maendeleo ya elimu nchini.

‎“Suala la lishe shuleni ni mtambuka kwani linahitaji ushiriki wa sekta na wadau mbalimbali ili kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula bora na huduma muhimu wanapokuwa shuleni,” alisema.

‎Aidha aliitaka Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI kuendelea kusimamia utekelezaji wa miongozo ya lishe shuleni pamoja na kuhakikisha vyakula na vinywaji vinavyouzwa katika maeneo ya shule vinakuwa salama na vinazingatia viwango vya afya ya umma.

‎"Ni muhimu kuimarisha usimamizi wa vyakula hivyo ili kulinda afya za watoto na kuhakikisha vinazingatia miongozo ya kimataifa ya afya,"alisisitiza.

‎Pia aliwataka wazazi kushirikiana na shule kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula wakiwa shuleni kama ilivyoelekezwa katika Waraka wa Elimu Na. 3 wa mwaka 2026, akibainisha kuwa ushirikiano huo utasaidia kuunda mazingira bora ya kujifunzia kwa wanafunzi.



Post a Comment

Previous Post Next Post