‎SERIKALI YAENDELEA KUFUNGUA FURSA KWA VIJANA SEKTA YA MADINI ‎

‎Na Edward Winchislaus.

‎Serikali imeendelea kuimarisha mikakati ya kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika sekta ya madini kwa kuwapatia leseni za uchimbaji, mafunzo ya kitaalamu pamoja na fursa za ajira.

‎Hatua hiyo inalenga kuhakikisha vijana wanashiriki moja kwa moja katika shughuli za utafutaji, uchimbaji na biashara ya madini ili kunufaika na rasilimali hiyo muhimu ya taifa.

‎Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mipango hiyo, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira wa Tume ya Madini, Mha. Hamis Kamando aliyemwakilisha Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini Mha. Ramadhani Lwamo, amesema serikali imeendelea kutenga maeneo maalum kwa wachimbaji wadogo ili kuongeza ushiriki wa vijana.

‎“Serikali imeendelea kutenga maeneo kwa wachimbaji wadogo katika mikoa mbalimbali ya kimadini ili kuwapa nafasi wananchi, hususan vijana, kushiriki katika shughuli za uchimbaji wa madini,” amesema Kamando.

‎Amesema hadi sasa jumla ya maeneo 65 yamependekezwa kutengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo katika mikoa mbalimbali nchini, huku sehemu kubwa ya wanufaika wakitarajiwa kuwa vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 45.

‎Kwa mujibu wa Kamando, katika kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka 2025 serikali ilitoa jumla ya leseni 5,983 za uchimbaji mdogo wa madini kwa Watanzania, sawa na asilimia 71 ya leseni zote zilizotolewa katika kipindi hicho.

‎Aidha, kupitia mradi wa Mageuzi katika Sekta ya Madini kwa Maendeleo Jumuishi na Endelevu (Mining for Better Tomorrow – MBT), leseni 273 zilitolewa kwa vikundi 183 vya vijana katika mikoa mbalimbali ya kimadini.



‎Hatua hiyo imewezesha vijana zaidi ya 2,550 kupata ajira za moja kwa moja katika shughuli za sekta ya madini zikiwemo uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini.

‎“Tunawahimiza vijana kufuatilia na kutumia fursa zinazotolewa na Tume ya Madini ili waweze kuwekeza na kunufaika na sekta ya madini,” amesema Kamando.

Post a Comment

Previous Post Next Post