Na Edward Winchislaus
Serikali imetangaza msimamo mkali wa kufanya mageuzi ya sheria zote zinazokwamisha maendeleo ya taifa, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Kauli hiyo imetolewa leo Machi 23,2026 na Waziri wa katiba na sheria Dkt.Juma Zuberi Homera wakati akifungua kikao cha nne cha Baraza la Nane la Wafanyakazi wa Wizara hiyo, kinacho jadili bajeti na mipango ya wizara.
Dkt. Homera, amesema wazi kuwa hakuna sheria itakayovumiliwa iwapo itakuwa kikwazo kwa utekelezaji wa mipango ya maendeleo. Akisisitiza kuwa serikali ipo tayari kufanya mapitio ya sheria ili ziendane na kasi ya mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.
"Kwahiyo sisi tumeweka utaratibu kuwa hakuna sheria itakayovumiliwa kama inakwamisha utekelezaji wa dira 2050 kwahiyo dhamira yetu ni kwamba sheria tutazibadilisha ili ziweze kwendana na na kasi ya utekelezaji wa dira 2050,"amesema.
Aidha,amesema kufikiwa kwa Dira ya 2050 kunategemea uwepo wa sheria imara lakini pia rafiki kwa maendeleo, akionya kuwa bila maboresho hayo, malengo ya taifa yanaweza kuchelewa kufikiwa. Hivyo, ameutaka mkutano huo kuhakikisha bajeti ya mwaka 2026/27 inaweka mkazo katika kuimarisha mfumo wa sheria na taasisi zake.
Katika kikao hicho, wajumbe wanajadili pia utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2025/26, wakitathmini mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zilizojitokeza. Lengo ni kuhakikisha rasilimali zinazotolewa zinatumika kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya kwa wananchi.
Kwa mwaka wa fedha 2026/27, wizara inatarajia kuimarisha utawala wa sheria, kuongeza upatikanaji wa haki kwa wakati na kupanua matumizi ya teknolojia katika huduma za kisheria. Hatua hizi zinatarajiwa kusaidia kuondoa urasimu na kuongeza ufanisi, huku zikiweka mazingira rafiki kwa maendeleo ya taifa.



Post a Comment