‎MKOA WA DODOMA WAJA NA SIKU TATU MAALUM ZA KUSIKILIZA NA KUTATUA KERO ZA WANANCHI

 


‎Na Edward Winchislaus.

‎Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Rosemary Senyamule  ametangaza kuanzishwa kwa siku tatu maalum za kusikiliza na kutatua kero za wananchi zitakazofanyika kuanzia tarehe 4 hadi 6 Machi 2026 katika eneo la Nyerere Square.

‎ Akizungumza na waandishi wa habari leo,machi 2,2026 mkuu wa mkoa  amesema lengo la mpango huo ni kuwasogezea wananchi huduma na kuwapa fursa ya kuwasilisha changamoto zao moja kwa moja kwa taasisi zote za umma zitakazoshiriki.

‎Amesema katika siku hizo kutakuwa na mambo matatu ya msingi. Kwanza, ni usikilizwaji na utatuzi wa kero za wananchi kwa kushirikisha taasisi zote za serikali mkoani Dodoma. Pili, kutolewa kwa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa kazi zilizofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya siku 100 za uongozi wake, ili wananchi wapate uelewa wa hatua zilizochukuliwa na serikali katika kuwaletea maendeleo.

‎Aidha, ameeleza kuwa kutakuwa na utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii bila malipo, ikiwemo upimaji wa presha na kisukari pamoja na ushauri wa afya.

‎ Mkuu huyo wa Mkoa ametoa wito kwa wananchi wote wa Dodoma kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo, huku akizitaka taasisi na watumishi wa umma kuhakikisha wanawajibika ipasavyo katika kusikiliza na kushughulikia kero. Pia amebainisha kuwa mkoa unapanga kuanzisha mfumo wa kudumu wa kupokea na kutatua kero kuanzia ngazi ya kitongoji hadi mkoa, utakaokuwa unatekelezwa kila mwisho wa mwezi.

Post a Comment

Previous Post Next Post