Mahakama ya Wilaya ya Babati katika shauri la Jinai Na. 2979/2026) imemtia hatiani Bw. Mohamed Twalib Baya aliyekuwa mhasibu, kwa kosa la kughushi sahihi za watia saini katika akaunti ya Zahanati ya Gidas na kuchukua fedha jumla ya shilingi 5,426,000 ambazo alizifanyia ubadhirifu.
Akisoma hukumu hiyo Mh. Victor Kimario Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Babati amemtia hatiani mshtakiwa, baada ya mshtakiwa huyo kufanya makubaliano (plea bargaining) na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Mshtakiwa amepewa adhabu ya kifungo baridi cha muda wa miezi mitatu pamoja kurejesha fedha alizozifanyia ubadhilifu kiasi cha Shilingi 5,426,000 kwa muathirika.
Hadi hukumu inasomwa mshtakiwa amerejesha kiasi cha Shilingi 5,426,000 katika akaunti ya Zahanati ya Gidas (Muhanga) iliyopo Bank ya NMB.
Shauri hilo lilikuwa linaendeshwa na waendesha mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Manyara, ambao ni Neema Gembe, Davis Masambu na Catherine Ngessy.

Post a Comment