‎FCC YACHOCHEA UWEKEZAJI WA MABILIONI, FURSA MPYA ZA AJIRA KWA VIJANA ZAONGEZEKA

 


‎Na Edward Winchislaus

‎Tume ya Ushindani nchini Tanzania imeendelea kuchangia ukuaji wa uchumi na kuleta fursa za ajira kwa vijana kupitia kuruhusu uwekezaji na miungano ya makampuni katika sekta mbalimbali katika mwaka wa fedha 2025/2026.

‎Hayo yameelezwa leo Machi 5,2026 jijini Dodoma  na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani, Bi.Khadija  Ngasongwa, wakati akiwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na mchango wa taasisi hiyo katika uchumi wa nchi.

‎Amesema katika sekta ya kilimo, Tume imeridhia uwekezaji wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 20.4, ikiwemo ununuzi wa kampuni ya Africado Limited inayojishughulisha na uzalishaji wa maparachichi kwa ajili ya masoko ya kimataifa. Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza uzalishaji wa kibiashara, kuimarisha ushirikiano na wakulima wadogo pamoja na kupanua masoko ya mazao ya kilimo nje ya nchi.


‎Aidha,Kwa upande wa sekta ya uzalishaji viwandani, Tume imeidhinisha miungano ya makampuni saba yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 103.9. Miungano hiyo inahusisha makampuni yanayozalisha bidhaa mbalimbali, zikiwemo sabuni, vifungashio, vifaa vya usambazaji maji na bidhaa za karatasi. Uwekezaji huu unatarajiwa kuongeza uzalishaji, kuimarisha ushindani wa soko na kuchochea ajira kwa Watanzania.

‎Katika sekta ya madini, Tume imeridhia uwekezaji mkubwa katika miradi ya Liganga na Mchuchuma pamoja na mradi wa madini ya ardhi adimu wa Ngualla. Miradi hiyo inatarajiwa kuvutia uwekezaji wa mabilioni ya dola za Kimarekani na kuzalisha mamia ya ajira za moja kwa moja pamoja na maelfu ya ajira zisizo za moja kwa moja wakati wa ujenzi na uendeshaji wa miradi hiyo.

‎Hata hivyo, Tume imeendelea kulinda walaji kwa kushughulikia malalamiko mbalimbali ya watumiaji na kudhibiti bidhaa bandia zinazoingia katika soko la Tanzania. Katika kipindi hicho, malalamiko 63 ya walaji yalishughulikiwa, huku juhudi za kutoa elimu kwa wadau na wananchi zikiendelea ili kuongeza uelewa kuhusu haki za mlaji na umuhimu wa ushindani wa haki katika biashara.

‎Kwa mujibu wa Ngasongwa, Tume pia imeanza utekelezaji wa mradi wa kidijitali wa kuboresha huduma zake kwa ushirikiano na TradeMark Africa pamoja na  kufungua ofisi mpya za kanda katika mikoa ya Arusha, Mwanza na Mbeya ili kusogeza huduma karibu zaidi kwa wananchi na wadau wa biashara nchini.


Post a Comment

Previous Post Next Post