Na Edward Winchislaus.
Wananchi wametakiwa kushiriki kikamilifu katika kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji ili kuhakikisha rasilimali hiyo muhimu inaendelea kuwepo kwa matumizi ya sasa na vizazi vijavyo.
Wito huo umetolewa leo Machi 6,2026 Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Dkt. Renatus Shinhu, ambaye amesema ulinzi wa rasilimali za maji haupaswi kuwa jukumu la serikali pekee bali unahitaji ushirikiano wa jamii nzima.
Amesema maji ni rasilimali muhimu kwa maisha ya binadamu pamoja na maendeleo ya kiuchumi, hivyo kila mwananchi anapaswa kutambua wajibu wake katika kuyatunza kwa kuepuka vitendo vinavyoweza kuharibu mazingira ya vyanzo vya maji.
Pia,Dkt. Shinhu ameeleza kuwa zamani jamii nyingi zilikuwa na mila na desturi zilizosaidia kulinda vyanzo vya maji, ambapo wananchi waliamini kuwa yeyote anayeharibu maeneo hayo angekumbwa na madhara, hali iliyosaidia kuyahifadhi kwa muda mrefu.
Hata hivyo, amesema kadri miaka ilivyopita baadhi ya mila na desturi hizo zimeanza kupotea, jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa vitendo vya uharibifu wa mazingira katika maeneo ya vyanzo vya maji.
Kutokana na hali hiyo, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuongeza uelewa kuhusu thamani ya maji na wajibu wa jamii katika kulinda rasilimali hiyo muhimu.
Aidha, amesema Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria inaendelea kuimarisha usimamizi wa rasilimali za maji kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali pamoja na nchi zinazozunguka bonde hilo kupitia jukwaa la kimataifa la Nile Basin Initiative.
Ameongeza kuwa kupitia ushirikiano huo, Tanzania imefanikiwa kujenga vituo vinane vya kisasa vya kufuatilia mwenendo wa maji katika baadhi ya vyanzo vinavyoingia Ziwa Victoria, ambapo vituo hivyo hukusanya takwimu za kila siku zinazosaidia wataalamu kupanga mikakati bora ya matumizi endelevu ya rasilimali za maji.



Post a Comment