Na Edward Winchislaus,Dodoma
Sekta ya madini imeendelea kuwa mhimili muhimu wa ajira na mapato nchini, huku Serikali ikifanikiwa kuongeza kiwango kikubwa cha ushiriki wa Watanzania katika migodi kupitia ajira, manunuzi ya bidhaa na huduma pamoja na mapato ya Serikali.
Mafanikio hayo yameelezwa leo Januari 5,2026 jijini Dodoma na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Waziri huyo amesema kuwa katika miradi ya madini, ajira kwa Watanzania zimeendelea kuongezeka kwa kiwango kikubwa, ambapo hadi Desemba 2024, ajira 6,668 kati ya ajira 7,003 zinashikiliwa na Watanzania, sawa na asilimia 97.Ambapo ameeleza kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuongeza idadi ya Watanzania wanaochukua nafasi zilizokuwa zikishikiliwa na wataalamu wa kigeni.
“Matokeo haya yanaonesha wazi kuwa sera na miongozo ya Serikali ya ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini inaendelea kuzaa matunda, na Watanzania sasa wanachukua nafasi muhimu katika ajira na uongozi wa migodi.
"katika miradi ya madini tumeshuhudia ongezeko la asilimia 95 kwa mwaka 2018 hadi kufikiaajira18,853 kati ya ajira 19,356
ajira kwa Watanzania kutoka ajira 6,668 kati ya ajira 7,003 sawa na sawa na asilimia 97 kufikia Desemba 2024",amesema.
Pia Waziri huyo ameutaja mgodi wa dhahabu wa North Mara, unaomilikiwa na Kampuni ya Twiga Minerals Corporation (Barrick Gold), kuwa mfano mzuri wa utekelezaji wa sera hiyo, akisema kuwa nafasi zote za juu za uongozi katika mgodi huo zinashikiliwa na Watanzania.
Aidha,Katika eneo la manunuzi ya bidhaa na huduma migodini, Mhe. Mavunde amesema Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini inaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Madini, Sura ya 123, kwa kuhakikisha kipaumbele kinatolewa kwa kampuni za Kitanzania huku akieleza kuwa manunuzi ya bidhaa na huduma kutoka kwa kampuni za Kitanzania yameongezeka kutoka Shilingi trilioni 1.85 mwaka 2018 hadi kufikia Shilingi trilioni 4.41 mwaka 2024, sawa na asilimia 88 ya manunuzi yote yaliyofanyika migodini.
"Usimamizi huo umekuwa na matokeo
chanya kwa kuongeza idadi ya Watanzania wanaotoa huduma na kuuza
bidhaa kwa wamiliki wa leseni za madini nchini",ameeleza.
Katika upande wa mapato ya Serikali, Waziri wa Madini anasema mapato yatokanayo na sekta ya madini yanaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka ambapo kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2020/2021 hadi 2024/2025, makusanyo yameongezeka kutoka Shilingi bilioni 526.7 hadi kufikia Shilingi trilioni 1.071, hali inayoonesha mchango mkubwa wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.



Post a Comment