Wafanyabiashara Machinga wachangamkia nyongeza ya muda wa uandikishaji
Na. Mwandishi Wetu, MAJENGO
Zoezi la uandikishaji kuelekea uchaguzi wa viongozi wa Soko la Wazi la Machinga umeingia katika sura mpya baada ya mamlaka inayosimamia uchaguzi huo kuongeza muda wa siku mbili kuanzia tarehe 14-16 Januari, 2026 kwa wafanyabiashara ambao hawakupata fursa ya kujiandikisha awali.
Hayo yameelezwa na Meneja wa Soko la Wazi la Machinga, CPA Johnstone Kahungu wakati akizungumza na waandishi wa habari waliofika katika soko hilo.
CPA. Kahungu alisema kuwa ongezeko la siku mbili za uandikishaji litawapa fursa wafanyabiashara ambao hawakupata nafasi ya kujiandikisha kwa mara ya kwanza. “Tulishafanya uandikishaji kwa awamu ya kwanza ambapo walijiandikisha wafanyabiashara 932 na lengo letu lilikuwa ni kuwaandikisha wafanyabiashara 2700. Baada ya kuona idadi hiyo bado ni ndogo tuliita kamati kwaajili ya kufanya tathimini na tukaona watu hawatoshi kwahiyo tukaamua tuongeze siku mbili ili wafanyabiashara ambao hawakujajiandikisha wapate fursa ya kujiandikisha. Uandikishaji unaendelea na wafanyabiashara wanajitokeza” alisema CPA. Kahungu.
Nae, Mfanyabiashara wa soko hilo Tryphone Katula alisema kuwa nyongeza ya muda imewapa nafuu kubwa wafanyabiashara waliokuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo majukumu ya kazi na uelewa mdogo wa awamu ya kwanza ya uandikishaji. “Tunaishukuru serikali na mamlaka za uchaguzi kwa kuongeza muda. Hii imetupa nafasi sisi tulioachwa nyuma kujiandikisha na kuwa sehemu ya maamuzi kwahyo nipende kuwashauri wafanyabiashara wenzangu waje wajiandikishe kwa kuwa tumeongezewa muda kwa sisi ambao hatukujiandikisha kwa mara ya kwanza” alisema Katula.
Kwa upande wake, mfanyabiashara mwingine Shida Samsoni alieleza kuwa ana furaha kupata fursa ya kujiandikisha. “Nimefurahi sana kwa kuongezewa muda wa siku mbili ili kwa sisi ambao hatukujiandikisha tuweze kujiandikisha. Nimepata fursa ya kujiandikisha, nawaalika pia wafanyabiashara wenzangu jiandikisheni ili tupate haki ya kupiga kura na kuchagua viongozi watakaosimamia maendeleo ya soko na mazingira ya biashara zetu” alisema Samsoni.
Zoezi la uchaguzi wa viongozi wa Soko la Wazi la Machinga limeongezewa muda ili kutoa nafasi kwa wafanyabiashara wote waliokosa nafasi ya kujiandikisha awamu ya kwanza kuhakikisha wanajiandikisha na kutimiza haki yao ya msingi ya kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia unaojumuisha haki ya kupiga kura.



Post a Comment