🔴 TFS yaungana na Ofisi ya Makamu wa Rais ( Muungano na Mazingira) kupanda miti mtumba.
Na Edward Winchislaus,Dodoma.
Maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, yamegeuka kuwa chachu ya kuimarisha utunzaji wa mazingira baada ya miti 693 kupandwa katika eneo la Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Zoezi hilo limefanyika ikiwa ni sehemu ya kuendeleza dhamira ya Rais Samia ya kulinda mazingira, ambapo siku yake ya kuzaliwa imetumika kuhamasisha upandaji wa miti kama hatua ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza katika tukio hilo, Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Festo Ndugange, amesema siku hiyo ni ya muhimu kwa taifa kwa kuwa Rais Samia ameendelea kuwa kinara wa utunzaji wa mazingira.
Dkt. Ndugange ameeleza kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais imeungana na Rais katika zoezi hilo kwa kupanda miti katika eneo lenye ukubwa wa takribani hekari 50 katika Mji wa Serikali Mtumba.
"waka 2017, Rais Samia akiwa Makamu wa Rais, alizindua rasmi bustani hii ya Mji wa Serikali, hivyo zoezi la sasa linaendeleza maono aliyoyaweka awali.,"amesema.
Aidha,amesisitiza kuwa misitu na mazingira ni uhai wa taifa, akibainisha kuwa endapo mazingira yatatunzwa, nayo yataendelea kuwalinda wananchi huku akiwahimiza wananchi kuendeleza utamaduni wa kupanda miti kila wanapoadhimisha siku muhimu, hususan siku za kuzaliwa, ili kuongeza kasi ya urejeshaji wa mazingira
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Abdallah Mitawi, amesema maadhimisho hayo yanaonesha kwa vitendo namna Rais Samia anavyojali masuala ya mazingira."Tuna mtakia Mhe.Rais afya njema tutaendelea kuhamasisha jamii kushiriki katika uhifadhi wa mazingira,"amesema
Naye Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Bw. Emanuel Wilfred Kiboko, amesema siku ya kuzaliwa kwa Rais imetumika mahsusi kuhamasisha upandaji wa miti kote nchini.
Pia,amesema Rais Samia ameendelea kuwa mhamasishaji namba moja wa uhifadhi wa mazingira, jambo lililosababisha siku yake ya kuzaliwa kubeba ujumbe wa kitaifa wa upandaji miti.
"Tukio hili limefanyika wakati muafaka ambapo mvua zinaendelea kunyesha katika maeneo mengi ya nchi, hali hii itasaidia miti iliyopandwa kustawi na kuimarisha ikolojia",amesema.
Amefafanua kuwa TFS inaendelea kutoa miche kwa wananchi kupitia ofisi za kanda na wilaya, huku ikifuatilia ili kuhakikisha miche hiyo inapandwa na kustawi.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Dodoma wamesema tukio hilo limeongeza uelewa na hamasa ya jamii kushiriki katika uhifadhi wa mazingira.Huku wakieleza kuwa kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya Rais kwa kupanda miti ni mfano wa uongozi wa vitendo unaopaswa kuigwa na viongozi na wananchi kwa ujumla.
Miti iliyopandwa katika eneo la Mtumba inajumuisha miti ya matunda, kivuli, miti asilia ya kutunza vyanzo vya maji pamoja na miti ya dawa, hatua inayolenga kulinda mazingira na kuacha urithi wa kijani kwa kizazi cha sasa na kijacho.








Post a Comment