‎SIKU 100 ZA DKT.SAMIA: TANZANIA YAPANDA RAMANI YA DUNIA YA MADINI ‎

Na Edward Winchislaus,Dodoma.

‎Katika kipindi cha siku 100 za uongozi wa Awamu ya Sita, Sekta ya Madini imeendelea kuwa mhimili muhimu wa mageuzi ya kiuchumi, huku Tanzania ikijiweka rasmi kwenye ramani ya dunia kama mzalishaji wa madini ya kimkakati na kuongeza hifadhi ya taifa ya dhahabu.

‎Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Januari 26, 2026, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema Serikali inatarajia kusaini mikataba mikubwa ya uchimbaji wa madini mapema Februari 2026, ikiwemo mradi wa niobium katika bonde la Songwe – Panda Hill, Mkoa wa Mbeya.

‎Amesema mradi huo utaambatana na ujenzi wa kiwanda cha kuongeza thamani kitakachozalisha Ferro-Niobium, hatua itakayoiingiza Tanzania miongoni mwa wazalishaji wakuu wa madini hayo duniani, nyuma ya Canada na Brazil. Mradi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya Shilingi trilioni 1 na kuzalisha maelfu ya ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.

‎Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde amesema kampuni ya kimataifa ya Barrick Gold iko tayari kuanza utafiti wa kina wa dhahabu katika wilaya za Nzega (Tabora) na Kahama (Shinyanga), hatua inayofungua fursa ya kuanzishwa kwa mgodi mpya mkubwa wa dhahabu nchini.

‎Kuhusu utafiti wa jiolojia, amesema Tanzania imefikia asilimia 97 ya utafiti wa msingi, asilimia 100 ya utafiti wa kimagnetiki na asilimia 24 ya jiokemia, huku Serikali ikilenga kufikia asilimia 50 ifikapo 2030, kwa mujibu wa Dira ya Sekta ya Madini: “Madini ni Maisha na Utajiri.”

‎Aidha, Waziri amebainisha kuwa katika kipindi cha miezi 14 tangu Oktoba 2024, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imenunua na kuhifadhi tani 17 za dhahabu, hatua iliyoiweka Tanzania kwenye nafasi ya 10 barani Afrika kwa hifadhi ya dhahabu, ikiipita nchi kadhaa zikiwemo Msumbiji.

‎Katika kuunga mkono agenda ya nishati safi, kupitia STAMICO, Serikali inatarajia kuzindua kiwanda cha mkaa mbadala wa Rafiki Briquettes mkoani Tabora, ambacho kitalenga kupunguza matumizi ya kuni na kusaidia shughuli za kilimo, hususan ukaushaji wa tumbaku.

‎Pia, ndani ya siku 100, Serikali imefanikiwa kufufua biashara ya madini ya vito kwa kufanikisha mnada wa kwanza wa madini ya vito jijini Arusha, kupitia ushirikiano wa Tume ya Madini na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).

‎Kwa hatua hizi, Sekta ya Madini inaendelea kuthibitisha nafasi yake kama nguzo ya uchumi wa taifa na chachu ya maendeleo endelevu chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.






Post a Comment

Previous Post Next Post