SERIKALI KUIMARISHA MAGEUZI YA ELIMU KUPITIA MATUMIZI YA TAKWIMU SAHIHI NA UPANUZI WA FURSA ZA MASOMO ‎

 


‎Na Edward Winchislaus

‎Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Serikali imejipanga kuimarisha mageuzi ya sekta ya elimu kwa kuzingatia matumizi sahihi ya takwimu, upanuzi wa fursa za masomo ya juu ndani na nje ya nchi, pamoja na utekelezaji wa elimu ya lazima ya miaka kumi.

‎Prof. Mkenda ameyasema hayo Januari 20, 2025, Jijini Dodoma, wakati akizungumza katika kikao kazi cha nusu mwaka cha Menejimenti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo.

‎Amesema kikao hicho ni cha kimkakati kwani kinatoa fursa ya kutathmini utekelezaji wa bajeti ya nusu mwaka na kuweka vipaumbele kwa mwaka wa fedha unaofuata, sambamba na kuimarisha utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo ya sekta ya elimu.

‎Katika hatua nyingine, Prof. Mkenda amebainisha kuwa Serikali inalenga kutumia kikamilifu fursa za ufadhili wa masomo (scholarships) zinazotolewa na nchi na taasisi mbalimbali za kimataifa ili kupunguza utegemezi wa mikopo ya elimu ya juu na kuongeza idadi ya Watanzania wanaonufaika na elimu.

‎Pia,amesema Tanzania imekuwa ikikosa kutumia ipasavyo fursa nyingi za ufadhili zinazopatikana nje ya nchi kutokana na changamoto za taarifa, uratibu na mifumo dhaifu ya ufuatiliaji. Ameeleza kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha fursa hizo zinawafikia na kuwanufaisha Watanzania wengi zaidi.

‎Aidha, Prof. Mkenda amesema Serikali ipo katika hatua za kuimarisha mfumo wa kitaifa wa takwimu za elimu utakaofuatilia mwenendo wa mwanafunzi kuanzia elimu ya awali hadi elimu ya juu au mafunzo ya ufundi. Amesisitiza kuwa mfumo huo utaisaidia Serikali kupata takwimu sahihi zitakazowezesha upangaji bora wa sera, bajeti na mipango ya maendeleo.

‎Ameongeza kuwa changamoto ya takwimu zisizo sahihi au zisizounganishwa imekuwa kikwazo katika kupanga mipango ya muda mrefu, hivyo Wizara inalenga kuwa na mfumo mmoja wa kitaifa unaounganisha taasisi zote za elimu, ikiwemo Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), NACTVET, vyuo vikuu na taasisi nyingine.

‎Kuhusu elimu ya lazima ya miaka kumi, Prof. Mkenda amesema Serikali inaendelea na maandalizi ya utekelezaji wake ili kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu hadi kidato cha nne bila vikwazo vya gharama, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Wizara, taasisi zake na wadau wa elimu.



‎Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amesema kikao hicho ni fursa muhimu ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mwelekeo wa utekelezaji wa sera na mipango ya Wizara.

‎Amesema Wizara itaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya viongozi, taasisi zake na wataalamu wa sekta ya elimu ili kuhakikisha mageuzi yanayopangwa yanatekelezwa kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya kwa Taifa.



‎Akitoa maelezo ya awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema kikao cha nusu mwaka ni sehemu ya utaratibu wa Wizara wa kutathmini utekelezaji wa majukumu yake na kupanga kwa pamoja hatua za utekelezaji kwa kipindi kijacho.

‎Ameongeza kuwa kikao hicho kinajadili utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo iliyoboreshwa, elimu ya kidijitali, utekelezaji wa bajeti, pamoja na upatikanaji wa fursa za elimu na ufadhili wa elimu ya juu, akisisitiza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya Wizara na taasisi zake ni msingi muhimu wa kufanikisha dira ya maendeleo ya Taifa kupitia sekta ya elimu.





Post a Comment

Previous Post Next Post