MTERA YAZIMA GIZAYAFUNGUA MILANGO YA VIWANDA DODOMA NA IRINGA,

 ‎MTERA YAZIMA GIZA, YAFUNGUA MILANGO YA VIWANDA DODOMA NA IRINGA


‎Na Edward Winchislaus.

‎Changamoto ya muda mrefu ya umeme hafifu na kukatika mara kwa mara katika maeneo ya Dodoma na Iringa sasa imeingia historia, baada ya Serikali kuzindua Kituo cha Kupoza Umeme cha Mtera, mradi mkubwa wa kimkakati unaolenga kuchochea uwekezaji wa viwanda, biashara na ajira kwa maelfu ya Watanzania.



‎Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuijenga Tanzania kuwa na uchumi wa kisasa, unaokua kwa kasi na wenye ushindani.

‎“Bwawa la Mtera lilianza kuzalisha umeme mwaka 1980 kwa megawati 80, lakini kwa zaidi ya miaka 40 hakujawahi kufanyika uwekezaji mkubwa kama huu tunaouona leo. Huu ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Waziri Ndejembi.

‎Pia,amesema kituo hicho kimejengwa mahususi kutatua changamoto za upatikanaji wa umeme katika wilaya za Mpwapwa na Kongwa mkoani Dodoma pamoja na Kilolo na maeneo ya Usmani mkoani Iringa, ambako kwa muda mrefu wawekezaji walikwamishwa na tatizo la low voltage.



‎Kwa mujibu wa Waziri huyo, hali ya awali iliwalazimu wamiliki wa viwanda vidogo kama mashine za kusaga na kukamua mafuta kusubiri umeme nyakati za usiku, hali iliyopunguza uzalishaji na kukatisha tamaa wawekezaji wakubwa.

‎“Leo hii mwekezaji anaweza kuwekeza bila hofu. Umeme wa uhakika unapatikana mchana na usiku, viwanda vinaweza kufanya kazi kikamilifu, ajira zinaongezeka na uchumi wa mwananchi mmoja mmoja unakua,” amesisitiza.

‎Hata hivyo,Kituo cha Kupooza Umeme cha Mtera kina uwezo wa kusambaza hadi megawati 18 za umeme, kiwango ambacho Waziri amesema baadhi ya mikoa nchini bado haijafikia kwa matumizi yake ya kawaida,ambapi ametoa wito kwa wananchi wa Dodoma na Iringa kujitokeza kwa wingi kuomba kuunganishwa na umeme na kuwa walinzi wa miundombinu hiyo.

‎Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Said, amesema mradi huo unalenga kusambaza umeme katika vijiji 121 ambavyo havikunufaika na mradi wa njia kuu ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga.

‎Aidha,ameeleza kuwa kabla ya ujenzi wa kituo hicho, umeme ulikuwa ukisafirishwa kwa zaidi ya kilomita 155 kutoka Kituo cha Zuzu, hali iliyosababisha upotevu mkubwa wa umeme na kukatika mara kwa mara.

‎“Mradi umehusisha ujenzi wa transfoma mbili za kupunguza umeme kutoka kilovolti 220 hadi 33 kwa ajili ya usambazaji. Kituo kina njia nne za kusambaza umeme, ambapo mbili ni za msongo wa kati wa kilovolti 33 zenye uwezo wa kupitisha hadi megawati 14 kila moja kwa Dodoma na Iringa,” alisema.

‎Ameongeza kuwa ujenzi wa kituo hicho umekamilika kwa asilimia 100 na tayari kinafanya kazi, ambapo upande wa Dodoma kwa sasa unapata megawati sita na Iringa megawati tatu, huku wawekezaji wanaotarajia kufungua viwanda na migodi wakiendelea kuunganishiwa umeme.

‎Mradi huo umegharimu Sh bilioni 9.7, ambapo asilimia 50 ya fedha zilitolewa na Serikali ya Sweden na asilimia 50 na Serikali ya Norway. Serikali imewashukuru wadau hao wa maendeleo kwa kuunga mkono juhudi za kuimarisha sekta ya nishati nchini.

‎Uzinduzi wa Kituo cha Kupoza Umeme Mtera unatajwa kuwa mkombozi wa uchumi wa maeneo ya kati na nyanda za juu kusini, ukiweka msingi imara wa ukuaji wa viwanda, ujasiriamali na ajira, na hivyo kuboresha maisha ya Watanzania wengi zaidi.

Post a Comment

Previous Post Next Post