MAVUNDE: TANZANIA NA MAREKANI ZIMEIMARISHA USHIRIKIANO UTAFITI WA MADINI MTWARA NA LINDI

 

‎Na Edward Winchislaus

‎Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema Tanzania na Marekani zimeendelea kuimarisha uhusiano wa muda mrefu wenye tija katika sekta ya madini, hatua inayolenga kukuza uchumi wa taifa, kujenga uwezo wa wataalamu wazawa na kuongeza thamani ya rasilimali za nchi.

‎Akizungumza na waandishi wa habari Januari 21, 2026 jijini Dodoma, Mhe. Mavunde amesisitiza kuwa Marekani imekuwa mshirika muhimu wa maendeleo ya Tanzania kwa miaka mingi, ikitoa msaada uliochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, ikiwemo sekta za afya, elimu, maji, kilimo, usalama wa chakula, miundombinu, demokrasia pamoja na rasilimali.

‎“Tanzania imenufaika kwa kiwango kikubwa na ushirikiano huu, na tunaishukuru Serikali ya Marekani kwa kuendelea kuwa nasi katika jitihada za kukuza uchumi na kuboresha maisha ya Watanzania,” amesema Mavunde.

‎Waziri huyo ameeleza kuwa kupitia Wizara ya Nishati na Madini ya Marekani, imeanzishwa programu maalum inayolenga kusaidia utekelezaji wa ajenda za maendeleo ya Tanzania, hususan katika sekta ya madini ambapo Tanzania imeendelea kutambulika kimataifa kama nchi yenye rasilimali nyingi za madini zenye mahitaji makubwa duniani.

‎Katika hatua ya kuimarisha ushirikiano huo, Wizara ya Madini ya Marekani imeanza kufanya kazi kwa karibu na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) pamoja na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), kwa lengo la kuimarisha utafiti wa pamoja na kujenga uwezo wa kitaalamu kwa Watanzania.

‎Aidha,Mavunde amefafanua kuwa zipo leseni za madini zinazomilikiwa na STAMICO ambazo zinafanyiwa utafiti wa pamoja ili kubaini maeneo yenye fursa kubwa za uwekezaji wa kimadini. Utafiti huo unalenga hasa mikoa ya Mtwara na Lindi, ambako matarajio ya kugunduliwa kwa migodi mikubwa yameongezeka.

‎“Ushirikiano huu umeonyesha dhamira ya dhati ya Tanzania na Marekani katika kuhakikisha rasilimali zetu zinatumika kwa manufaa ya pamoja. Kupitia utafiti wa kina, tunatarajia kubaini maeneo yenye utajiri mkubwa wa madini na hatimaye kupata migodi mikubwa itakayochochea maendeleo ya kiuchumi,” amesema.


‎Vilevile,ameongeza kuwa Serikali ya Marekani imeonyesha utayari wa kushirikiana na Tanzania katika kuongeza maeneo yanayofanyiwa utafiti wa kina nchini, sambamba na kutoa mafunzo yatakayowawezesha Watanzania kusimamia rasilimali zao kwa ufanisi na weledi zaidi.

‎Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, maeneo yanayofanyiwa utafiti wa kina yamebainika kuwa na madini kimkakati ya kinywe, ambayo mahitaji yake duniani yanatarajiwa kufikia tani milioni 4.5 kwa mwaka ifikapo 2050. Hali hiyo imeiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuwa miongoni mwa wasambazaji wakuu wa madini hayo katika soko la dunia.

‎Sambamba na utafiti huo, yameandaliwa mafunzo ya siku mbili kwa wataalamu wa Kitanzania, yakilenga matumizi ya teknolojia ya kisasa ya hali ya juu katika uchambuzi na tafsiri ya takwimu za kimadini ambapo Mavunde amesema vifaa vitakavyokabidhiwa vitaongeza uwezo wa wataalamu wa ndani kupata na kutafsiri taarifa sahihi za utafiti.

‎“Ninapenda kusisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Marekani katika maeneo mbalimbali, hususan sekta ya madini, ili kuhakikisha nchi zote mbili zimenufaika na rasilimali hizi huku tukijengeana uwezo kulingana na mahitaji ya sasa na ya baadaye,” amesisitiz Waziri Mavunde.



‎Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andrew Lentz, alisema Serikali ya Marekani itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali, ikiwemo sekta ya madini, ili kuhakikisha utafiti wa kina unafanyika na fursa za uwekezaji zinabainishwa kwa manufaa ya pande zote.

‎“Kwa kushirikiana na STAMICO, tutafanya utafiti wa kiwango cha upatikanaji wa madini ya kinywe katika mikoa ya Lindi na Mtwara pamoja na kuwajengea uwezo Watanzania kuhusu mchakato mzima wa utafiti,” alisema Lentz.

‎Alisisitiza kuwa ushirikiano huo una lengo la kusaidia Tanzania kuongeza thamani ya rasilimali zake, kuvutia uwekezaji mkubwa na kuchangia katika ukuaji wa uchumi endelevu.




Post a Comment

Previous Post Next Post