Na Edward Winchislaus,Dodoma.
Serikali imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha biashara ya senene kwa kuwapatia wafanyabiashara masoko ya uhakika, kuboresha miundombinu pamoja na kuweka mazingira wezeshi yatakayochochea ukuaji wa sekta hiyo muhimu katika Mkoa wa Kagera.
Kauli hiyo imetolewa leo Januari 30, 2026 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, wakati akijibu swali la Mbunge wa Bukoba Mjini, Mhe. Johnston Mutasingwa, katika kipindi cha maswali na majibu cha Bunge la 13, Mkutano wa Pili, Kikao cha Nne.
Akijibu swali la msingi, Mhe. Londo amesema serikali inaendelea kufungua masoko ya uhakika ya bidhaa za senene katika miji mikubwa nchini na nje ya nchi, sambamba na kuwashirikisha wafanyabiashara katika maonesho ya biashara ya kikanda na kimataifa.
Amesema senene zinaendelea kutangazwa kama bidhaa mahsusi ya Ukanda wa Ziwa Victoria yenye uwezo wa kuingia katika masoko ya nchi tano za Afrika Mashariki na kwingineko.
“Serikali kupitia SIDO kwa kushirikiana na COSTECH pamoja na VETA inaendelea kufanya tafiti mbalimbali ili kuendeleza na kuboresha biashara ya senene, hususan katika Mkoa wa Kagera,” amesema Mhe. Londo.
Katika maswali ya nyongeza, Mhe. Mutasingwa ameeleza changamoto ya wafanyabiashara zaidi ya 1,000 wa senene katika Jimbo la Bukoba Mjini kukosa maeneo rasmi ya kufanyia biashara zao, huku eneo walilokuwa wakitumia likijengwa kituo cha mabasi, na kuomba serikali itenge fedha ili kujumuisha eneo maalum kwa wafanyabiashara hao.
Akijibu, Naibu Waziri amesema serikali kwa kushirikiana na Manispaa ya Bukoba Mjini imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Soko la Senene (Senene Complex) katika soko la mjini, mradi unaolenga kuwakusanya wafanyabiashara hao katika eneo moja lenye miundombinu rafiki na salama.
Kuhusu uwezeshaji wa kifedha, amesema suala hilo linatarajiwa kuingizwa kama ombi maalum katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 kupitia serikali za mitaa, huku Wizara ya Viwanda na Biashara ikiahidi kushirikiana kikamilifu kuhakikisha biashara ya senene inapewa msukumo unaostahili.
Katika hatua iliyopokelewa kwa shangwe, Mhe. Londo pia ameahidi kuambatana na Mbunge wa Bukoba Mjini mara baada ya Bunge kumalizika kwenda Bukoba, ili kujionea hali halisi na kuzungumza moja kwa moja na wafanyabiashara wa senene.
Hatua hiyo inaonesha dhamira ya serikali ya kusikiliza na kutatua changamoto za wafanyabiashara wadogo, huku biashara ya senene ikitazamwa kama fursa muhimu ya ajira, kipato na uchumi wa wananchi wa Bukoba na Kagera kwa ujumla.



Post a Comment