‎DKT. MIGIRO ATOA MAAGIZO MAZITO: VIONGOZI WARUDI MASHINANI ‎

 

‎Na Edward Winchislaus, Dodoma

‎Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Asha Rose Migiro, ametoa maagizo kwa viongozi wa chama katika ngazi zote kurejea kwenye mashina, matawi na kata ili kuimarisha utekelezaji wa ahadi za chama na kutatua changamoto za wananchi moja kwa moja.

‎Akizungumza leo Januari 20,2026  jijini Dodoma katika mkutano wa mabalozi wa mashina mkoa wa Dodoma,Dkt. Migiro amesema ushindi mkubwa uliopatikana kwenye uchaguzi ni mwanzo wa kazi kubwa ya kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi, akisisitiza kuwa utekelezaji huo lazima uanze kwenye mashina.

‎“Tayari tumekamilisha uchaguzi na tumepata ushindi mnono,kazi iliyopo sasa ni kuubadilisha ushindi huo kuwa utekelezaji wa ahadi na maendeleo kwa wananchi, na hilo litaanzia mashinani,” amesema.

‎Katibu Mkuu huyo ameagiza viongozi ambao hawajafanya vikao katika mashina kuhakikisha wanafanya vikao hivyo mara kwa mara, akibainisha kuwa mashina ndiyo ngazi sahihi ya kubaini changamoto za wananchi na kuziwasilisha ngazi za juu kwa ufumbuzi.

‎Aidha,amesisitiza kuwa mashina siyo sehemu ya wakereketwa pekee, bali ni jukwaa la wananchi wote, wanachama na wasiokuwa wanachama wa CCM, kwa ajili ya kujadili maendeleo ya jamii na masuala yanayohusu taifa.

‎Kwa mujibu wa Dkt. Migiro, viongozi wanapaswa kutumia mashina kama sehemu ya kutangaza utekelezaji wa ilani ya CCM, kusikiliza kero za wananchi na kuzigeuza kuwa fursa za maendeleo.

‎“Viongozi wetu wa juu warudi mashinani, tufanye vikao, tukusanye hoja na maoni, na tuyapeleke ngazi za juu. Hapo ndipo tutajenga chama chenye nguvu na taifa imara,” amesema.

‎Vilevile, ameagiza mashina ya CCM yawe ngome ya ulinzi wa chama na sehemu ya kuandaa viongozi wa baadaye, akisisitiza kuwa huko ndiko kunakoonekana kwa karibu mwenendo wa jamii na ulinzi wa maslahi ya taifa.

‎Katika maagizo yake, Dkt. Migiro amewataka viongozi kuwa makini katika kuunganisha maamuzi ya chama, kuwasilisha sera zenye kuleta mshikamano na kutumia changamoto zinazojitokeza kama fursa ya kuimarisha CCM.

‎Kwa upande wake, Mbunge wa Mtumba na Waziri wa Madini, Mhe.Anthony  Mavunde akitoa shukurani kwa niaba ya wabunge waliyo hudhuria kikao hicho amesema mabalozi wa mashina wamepokea maagizo hayo na wako tayari kuyatekeleza kwa vitendo kwa kushirikiana na wananchi.




Post a Comment

Previous Post Next Post