Na Edward Winchislaus,Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, ameongoza kikao cha Ushauri wa Maendeleo ya Mkoa (RCC) kilicholenga kuweka mwelekeo na mikakati ya maendeleo ya mkoa huo kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao na mipango ya miaka mitano ijayo.Kikao hicho kimewakutanisha wabunge wa mkoa, viongozi wa vyama vya siasa,viongozi wa dini, kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa,wakuu wa taasisi pamoja na wadau kutoka sekta mbalimbali za maendeleo.
Katika kikao hicho, wajumbe walipokea mawasilisho ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa kipindi kilichopita na mipango ya sekta mbalimbali kwa mwaka mmoja ujayo, kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na mwelekeo wa serikali ya Awamu ya Sita.
“Kikao hiki ndicho kikao kikubwa kuliko vyote kwa ngazi ya mkoa kwani sasa tunaanza rasmi safari ya miaka mitano mingine ya kupanga maendeleo ya mkoa wetu kwa kuzingatia dira ya 2050,” amesema Mhe. Senyamule alipokuwa akifungua kikao hicho.
Mhe. Senyamule amepongeza mafanikio yaliyopatikana katika miaka iliyopita, akisema mkoa wa Dodoma umeendelea kupiga hatua katika sekta za kijamii na kiuchumi huku akitaja maboresho ya huduma za afya kwa kuongeza watumishi wa Afya, ujenzi wa miundombinu katika sekta ya elimu pamoja na kuimarika kwa upatikanaji wa nishati vijijini.
Amesema mafanikio hayo yamechangia kuongeza fursa za maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi wa Dodoma.
“Tumeshuhudia mabadiliko makubwa katika sekta ya afya, elimu na nishati, na sasa karibu kila kijiji kimeunganishwa na umeme,” amesema.
Akizungumzia vipaumbele vya mwaka mmoja ujao na mpango wa miaka mitano ijayo, Mkuu wa Mkoa amesema uchumi wa Dodoma utaimarishwa kupitia kilimo cha kisasa na matumizi ya teknolojia ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi ambapi amebainisha kuwa mkazo utawekwa pia katika kuimarisha lishe na uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Ameongeza kuwa sekta ya utalii ni fursa muhimu kwa maendeleo ya mkoa kutokana na vivutio vya kipekee vilivyopo Dodoma, ikiwemo zao la zabibu na utalii wa utamaduni wa jamii za mkoa huo.
“Dodoma ina vivutio ambavyo huwezi kuvipata sehemu nyingine, kama utalii wa zabibu na ngoma za asili za kigogo, na tukiviendeleza tutafungua fursa nyingi za ajira na kipato,” alisema.
Mhe. Senyamule ameeleza pia dhamira ya kuifanya Dodoma kuwa mkoa wa kimkakati katika usafiri na usafirishaji, pamoja na kuendelea kuimarisha sekta ya viwanda, biashara, madini na michezo, ikiwemo ujenzi wa uwanja mkubwa wa michezo wa kimataifa Nzuguni.
Kwa upande wa utekelezaji wa mipango ya kiuchumi, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Aziza Mumba, amesema mkoa ulikumbwa na changamoto ya mvua chache katika msimu wa 2024/25, hali iliyosababisha uzalishaji wa kilimo kushuka.
“Baadhi ya maeneo yalipata mvua chini ya milimita 300 badala ya matarajio ya milimita 500 hadi 800, hivyo uzalishaji ulifikia asilimia 50 pekee ya lengo,” amesema.
Ameongeza kuwa licha ya changamoto hiyo, serikali imeendelea kuchukua hatua za kimkakati ikiwemo kuwekeza kwenye miradi mikubwa ya umwagiliaji katika wilaya mbalimbali za mkoa huo.
“Kwa mwaka 2025/26 tumepanga kulima hekta 800,000 na tunatarajia kuzalisha tani milioni 1.6, huku miradi ya mabwawa, visima na skimu za umwagiliaji ikiendelea kutekelezwa,” alifafanua.

Post a Comment