Na Edward Winchislaus.
Diwani mpya wa Kata ya Mnadani jijini Dodoma, Mhe. Mugendi Karenge, leo amekabidhiwa rasmi ofisi yake siku moja baada ya kuapishwa, na kutoa wito wa ushirikiano kwa watendaji na wananchi ili kuharakisha maendeleo katika kata hiyo.
Akizungumza mara baada ya kupokelewa ofisini hapo Disemba 5.2025 Mhe. Karenge amesema maendeleo ya kweli yatapatikana endapo viongozi na wananchi watadumisha umoja, mshikamano na uwajibikaji.
“Ili tulete mabadiliko ndani ya Kata ya Mnadani, lazima tuwe pamoja. Tukishirikiana hakuna jambo litatushinda,” alisema.
Ameongeza kuwa changamoto zinazowakabili wananchi zitaanza kupungua mara tu kila kiongozi na mtendaji atakapotimiza wajibu wake kikamilifu huku akionya Watendaji Wenye Lugha Chafu,na kuwaelekeza watendaji hao kutoa huduma kwa weledi na nidhamu, akipinga vikali matumizi ya lugha zisizofaa kwa wananchi.
“Kiongozi akishindwa kutatua kero fulani, ni bora awe mkweli amuelekeze mwananchi sehemu sahihi ya kupata ufumbuzi. Sitaki kusikia malalamiko ya lugha mbaya kutoka kwa viongozi wangu,” alionya.
Kuhusu fursa za kiuchumi, Mhe. Karenge amesema amepokea tangazo la mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wajasiriamali ambapo amemwagazib mtendaji wa kata hiyo kuhakikisha vikundi vyote vilivyosajiliwa vinapata taarifa hizo bila ubaguzi huku akibainisha kuwa kufikia Desemba 15 mwaka huu anatarajia vikundi vyote viwe tayari vimewasilisha maombi ya mikopo hiyo.
Kwa upande wake Katibu wa CCM Kata ya Mnadani, Bw. Athumani Malatu, amesema wananchi wana imani kubwa na uongozi wa Mhe. Mugendi, akiahidi kuwa chama kitatoa ushirikiano wa kutosha ili kutekeleza ilani na ahadi za maendeleo zilizotolewa kwa wananchi wakati wa kampeni.
Naye Diwani mstaafu wa kata hiyo, Dkt. Steven Augustin, amempongeza diwani mpya na kumhakikishia kuwa yuko tayari kumpa ushirikiano ili kuhakikisha malengo ya maendeleo yanafikiwa.
Hakika siku ya leo imemfungulia ukurasa mpya wa matumaini kwa wananchi wa Kata ya Mnadani, Kauli za Mhe. Mugendi zimeonesha dira ya uongozi unaoweka mbele uwajibikaji, ushirikiano, na huduma kwa wananchi. Wengi wanaamini kuwa sura mpya ya maendeleo inaanza kuonekana katika kata hiyo.

Post a Comment