Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chamwino, Tito Mganwa, amesema halmashauri imeanza rasmi zoezi la upimaji ardhi katika kata za Buigiri na Chamwino, akieleza kuwa zaidi ya hekari 1,000 zinatarajiwa kupimwa kwa lengo la kurasimisha umiliki wa ardhi, kulinda vyanzo vya maji na kupunguza migogoro ya ardhi, huku akisisitiza kuwa zoezi hilo linafuata misingi ya kisheria na mipango ya maendeleo ya mji wa Chamwino.
Amesema halmashauri imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa upimaji na urasimishaji wa ardhi, akifafanua kuwa wananchi watakaopimiwa na kushindwa kulipia gharama za upimaji watalipwa fidia stahiki bila dhuluma yoyote, hatua inayolenga kuhakikisha haki, usawa na ulinzi wa maslahi ya wakazi wote wa maeneo husika.
Wakizungumza kuhusu zoezi hilo, baadhi ya wakazi wa kata ya Buigiri wameupongeza uongozi wa Halmashauri ya Chamwino kwa kuona umuhimu wa kupima ardhi, wakisema hatua hiyo itasaidia kuondokana na migogoro ya ardhi, kudhibiti ujenzi holela na kuwezesha matumizi bora ya ardhi kwa maendeleo ya wananchi.
Mmoja wa wamiliki wa mashamba kata ya Buigiri, Keneth Willison, amesema ni furaha kubwa kwa wakazi wa eneo hilo kupata mradi wa upimaji ardhi baada ya maeneo yao kwa muda mrefu kushindwa kupimwa kutokana na hoja za kuwa ni maeneo ya bonde na vyanzo vya maji, hali iliyozuia matumizi yake kikamilifu.
Naye mkazi wa Buigiri, Elizabeth Mtomo, amesema kuanza kwa zoezi la upimaji ardhi kutasaidia kupatikana kwa mpangilio mzuri wa makazi, biashara na taasisi, huku akiwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi la upimaji na urasimishaji wa ardhi ili kupata umiliki halali na kuweka msingi wa maendeleo endelevu.

Post a Comment