WMA' DODOMA YATAKA WAUZAJI WA GESI KUHAKIKISHA MATUMIZI SAHIHI YA MIZANI

 


‎Na Edward Winchislaus.

‎Wakala wa Vipimo (WMA) mkoa wa Dodoma umeendelea kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya vipimo kwa wauzaji wa gesi, wakiwemo wauzaji wakubwa, wadogo na mawakala wa kusambaza mitungi ya gesi za majumbani,ambapo mafunzo hayo yamefanyika jijini Dodoma Novemba 22, 2025, yakilenga kuhakikisha bidhaa zinazowafikia wateja zinakuwa na ujazo halisi.

‎Akizungumza katika mafunzo hayo, Meneja wa Wakala wa Vipimo mkoa wa Dodoma, Bw. Said Ibrahim, amesema kutokana na  ongezeko la matumizi ya gesi ya kupikia nchini, hivyo ni muhimu kwa wauzaji kuhakikisha wanatumia mizani sahihi na iliyohakikiwa.

‎“Ni muhimu wauzaji wa gesi kuhakikisha kuwa gesi wanayouza au kununua kwa ajili ya biashara ina ujazo sahihi. Ili kufanikisha hili, lazima watumie mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo, yenye nembo na maelezo yanayoonyesha tarehe ya uhakiki na lini utarudiwa,” alisema.

‎Amesema uhakiki wa mizani hufanywa kila mwaka ikiwa ni  pamoja na ukaguzi wa kushtukiza, ili kuzuia mianya ya udanganyifu na kulinda haki ya mlaji na mfanyabiashara mwenyewe.

‎Pia Bw. Ibrahim aliwataka  wananchi kuzoea kupimiwa gesi wanaponunua, akibainisha kuwa baadhi ya changamoto zinazojitokeza ni wateja kutoomba kupimiwa gesi hizo, jambo linaloweza kuwapa nafasi baadhi ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu kuuza ujazo pungufu.

‎Kwa upande mwingine, baadhi ya wauzaji na wasambazaji wa mitungi ya gesi wameeleza uzoefu wao katika matumizi ya mizani, huku wakisema mafunzo hayo yamewapa mwanga kuhusu namna bora ya kuhudumia wateja.

‎Akizungumza katika mafunzo hayo, Mrakibu Msaidizi,Afisa habari  mawasiliano na elimu kwa umma kutoka  Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Dodoma,ASF.Stephen Katte  aliwataka wauzaji wa gesi kufuata taratibu na kupata vibali vinavyotakiwa kisheria ili kuepuka adhabu mbalimbali.

‎Kuhusu usafirishaji wa gesi, mrakibu huyo alionya juu ya matumizi ya magari yasiyo rasmi kusafirisha mitungi ya gesi, akisema hatua hiyo ni hatari na imesababisha matukio mbalimbali ya milipuko.

‎“Magari ya kubebea mitungi ya gesi yanatakiwa kuwa yamefungwa juu, kuwa na keji na sakafu maalum ili kuzuia mitungi kuchubuka. Siku hizi watu wanabeba mitungi kwenye pikipiki aina ya toyo na guta, jambo linaloweza kusababisha madhara makubwa endapo mtungi utalipuka,” alisema.

‎Washiriki wa mafunzo hayo, ambao ni wauzaji na wasambazaji wa gesi, walipongeza juhudi za Wakala wa Vipimo, wakisema elimu waliyoipata itawasaidia kuboresha huduma na kuongeza uaminifu kwa wateja.

‎Mafunzo kama hayo hutolewa mara kwa mara na Wakala wa Vipimo katika mikoa mbalimbali nchini, kwa lengo la kulinda haki ya mlaji na kuhakikisha bidhaa zinazohitaji vipimo sahihi, zikiwemo gesi za kupikia, zinauzwa kwa mujibu wa sheria na kanuni.

Post a Comment

Previous Post Next Post