Na Edward Winchislaus.
Tume ya haki za binadamu na utawala bora (THBUB) imelaani matukio ya mauaji ya wananchi yaliyojitokeza katika kipindi cha uchaguzi mkuu wa oktoba 29,2025 katika baadhi ya mikoa hapa nchini.
Tamko hilo limetolewa leo Novemba 5,2025 jijini hapa Dodoma na mwenyekiti wa tume hiyo Mhe.Jaji mstaafu Methew Mwaimu wakati akitoa tamko la tume hiyo kwa umma,ambapo amesema matukio hayo hayapaswi kuungwa mkono kwani yanavunja haki za binadamu.
Amesema mbali na tukio hilo la vifo,kufuatia maandamano hayo yalisababisha uharibifu wa mali za umma na mali za wananchi kama uchomaji wa vituo vya mafuta,uchomaji wa magari na majengo ya wananchi huku akisema kua matukio hayo yalipelekea baadhi wanchi kuhofia usalama wao.
“Tume ya haki za binadamu na utawala bora haikufurahishwa na matukio hayo na tunalaani matukio yaliyosababisha uvunjifu wa amani,vilevile matukio haya yaliweza kuvunja haki za baadhi ya watu na raia wema waliyokuwa katika shughuli za utafutaji wa riziki zao.
“Kwa namna yeyote ile matukio yote hayo hayapaswi kuungwa mkono kwasababu yanavunja amani katika nchi na usalama kiujumla,”amesema.
Aidha tume hiyo imesema kufuatia matukio hayo imeendelea kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini maeneo yaliyoathiriwa na matukio hayo ili iweze kutoa ushauri kwa serikali na kuendelea kulinda amani katika Taifa letu.
“katika kipindi kama hiki na matukio yaliyojitokeza kumevunjwa baadhi ya haki za wananchi kwasababu baadhi ya wananchi wamepoteza maisha wengine wamepoteza mali na wengine mali zao zimeharibiwa kwahiyo sisi kama tume tumeona ni matukio tunayopaswa kuyafanyia uchunguzi ili tuweze kutoa ushauri kwa namna ya kuweza kuondokana na matukio kama haya katika kipindi kingine cha uchaguzi,”amesema.
Sambamba na hayo tume imewahimiza wananchi kote nchini kuendelea kutunza tunu ya amani kwa kuzingatia misingi ya katiba na kanuni za nchi kwani inapotokea uvunjifu wa amani kila mmoja anashindwa kufanya shughuli zake za kila siku.

Post a Comment