Mbunge wa Jimbo la Mtumba, Anthony Mavunde, amekabidhi vifaa mbalimbali vya TEHAMA kwa shule za msingi na sekondari ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kupunguza mzigo wa michango ya mitihani ambayo wazazi walikuwa wakitozwa kila Jumamosi.
Katika hafla hiyo, Mavunde amekabidhi mashine za fotokopi kwa kata 20, kompyuta mpakato 20 kwa waratibu elimu kata na kompyuta mpakato 90 kwa walimu wakuu na wakuu wa shule za Serikali katika Jimbo la Mtumba.
Amesema vifaa hivyo vitasaidia kuongeza ufanisi katika maandalizi ya mitihani, ufundishaji na usimamizi wa elimu, hatua itakayopunguza mzigo kwa wazazi na kuongeza ufaulu wa wanafunzi.
Aidha, amewataka walimu kuimarisha umoja na ushirikiano ili kukabiliana na upungufu wa walimu katika baadhi ya masomo, sambamba na kuongeza kasi ya kuinua kiwango cha elimu jimboni humo.
Mbunge huyo ameahidi kuendelea kuboresha mazingira ya elimu, huku akitangaza mpango wa kuanzisha SACCOS ya walimu wa Jimbo la Mtumba, ambayo atawekea shilingi milioni 20 kama mtaji wa kuanzia ili kuwawezesha walimu kiuchumi.
“Tutashirikiana na Serikali kujenga miundombinu bora na kutatua changamoto katika sekta ya elimu, kwa kuwa elimu ndiyo kipaumbele chetu kikubwa,” alisema Mavunde.
Vilevile, ameahidi kuendeleza vipaji vya watoto kupitia Shindano la Mavunde na kuanzisha mashindano mengine ndani ya jimbo hilo ili kukuza uwezo wa wanafunzi katika nyanja mbalimbali.
Akizungumzia mchango wake kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu, Mhe. Mavunde alisema tayari ameanzisha Mavunde Foundation, yenye lengo la kuwawezesha watoto kupata elimu na kujikwamua kimaisha.
Ametoa wito kwa walimu wakuu na waratibu elimu kata kuhakikisha vifaa walivyokabidhiwa vinatunzwa na kutumiwa ipasavyo ili kutatua changamoto za elimu na kupunguza gharama kwa wazazi.
Kwa upande wake, Mratibu wa Programu ya BOOST kutoka OR-TAMISEMI, Reuben Swilla, amempongeza Mhe. Mavunde kwa kuanza kutekeleza ahadi zake mapema, akibainisha kuwa ni siku ya tano tu tangu aapishwe na tayari ameanza kuleta mabadiliko yenye tija jimboni.
Swilla amewataka watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuunga mkono juhudi hizo za Serikali na Mbunge wao ili kuendelea kuboresha elimu. Amesema hatua hiyo imeifanya Mtumba kuwa miongoni mwa majimbo yanayoelekea kuwa na shule za kisasa, kwani shule zote zinakwenda kuunganishwa na TEHAMA katika kufundisha na kujifunza.
“Kwa hili ulilolifanya, si tu umeisaidia Serikali kuboresha elimu, bali pia umepunguza kero ya michango kwa wazazi. Hatimaye, watoto wote wa Jimbo la Mtumba sasa watafanya mitihani bure kila Jumamosi,” alisema Swilla.

Post a Comment