‎CCM YAWAKALIA KOONI VIONGOZI WAZEMBE WAKIWEMO MAWAZIRI,YATANGAZA KUISIMAMIA SERIKALI

 



Na Edward Winchislaus.

‎Leo Jumatano Novemba 19.2025  jijini Dodoma, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndg.Kenani Kihongosi, amefanya mkutano na  waandishi wa habari na kutoa msimamo mzito kuhusu namna chama kitakavyosimamia utendaji wa serikali katika kipindi hiki.

‎Akizungumza katika mkutano huo, Kihongosi amesema kuwa CCM, kama chama kinachoongoza dola, kina wajibu wa kuhakikisha serikali inatekeleza kikamilifu ilani ya chama hicho na ahadi ilizotoa kwa wananchi. Huku akisisitiza kuwa usimamizi wa chama kwa serikali ni sehemu muhimu ya kuhakikisha maendeleo yanawafikia Watanzania kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili.

‎"wajibu wetu kama chama cha mapinduzi  ni kwenda kuisimamia serikali na siyo serikali kwenda kukisimamia chama cha mapinduzi ambacho kimetafuta kura, ambacho kimeunda serikali,sasa tunakwenda kuisimamia serikali kikamilifu,"amesema.

‎Katika hatua nyingine Kihongosi  ametoa onyo kali kwa viongozi wa serikali watakaoshindwa kutimiza majukumu yao akisema  kuwa chama hakitasita kuchukua hatua kali kwa viongozi wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa, uzembe au kutowajibika kwa namna yoyote ile.

‎"Wateuliwa wote waende wakawajibike kwasababu chama hakitasita kumchukulia hatua kiongozi yeyote wa serikali awe mteuliwa au amechaguliwa ambaye atakwenda kufanya kazi kwa maslahi yake binafsi chama kitamchukulia hatua,"amesisitiza.

‎Mkutano huo umeweka bayana dhamira ya CCM kuendelea kusimamia mwelekeo wa serikali, kuhakikisha viongozi wanafanya kazi kwa maslahi ya wananchi na kulinda heshima ya chama na taifa kwa ujumla.

Post a Comment

Previous Post Next Post