Na Suzana Alex
Kuelekea uchaguzi mkuu Watanzania wameshauriwa kujihadhari na mitandao feki ya kijamii inayopotosha taarifa na kupelekea kutoweka kwa amani na utulivu nchini.
Rai hiyo imetolewa na Mwanasheria wa Machifu Tanzania,Samwel Chimanyi alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma na kueleza kuwa watanzania wasikubali kupotoshwa na taarifa zitakazotolewa za matokeo ya uchaguzi siku ya kupiga kura bali taarifa sahihi watazipata kutokea kwenye mamlaka husika ambayo ni Tume Huru ya Taifa ya uchaguzi si kwingine.
Amesema kuwa kuna watu wametengeneza mifumo feki kwenye mitandao ya kijamii ambayo imekuwa ikitoa taarifa za upotoshaji na zenye kutishia amani na utulivu hasa kwenye kipindi hiki cha uchaguzi.
"Niwaombe vijana imarisheni maadili yenu mliyonayo kwa mujibu wa mila na desturi za mtanzania alizonazo,jiepusheni kutumiwa kama madarakia ya kupitia kwa baadhi ya wanasiasa ambao wasioitakia Nchi kuwa na uchaguzi wenye amani na utulivu"amesema Chimanyi
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wanawake na Samia Mkoa wa Dodoma Fatuma Madidi amewaomba akina mama kuhakikisha wanatoa elimu kwa wengine juu ya madhara yanayotokea pindi Nchi inapokuwa na machafuko baada ya kukosa amani na utulivu.
Madidi amesema kuwa mara nyingi inapotokea machafuko yoyote ndani ya Nchi wahathirika wakubwa ni watoto,wanawake na watu wenye ulemavu,hivyo kuelekea kwenye uchaguzi mkuu unaofanyika mwaka huu suala la amani liwe ni ajenda ya kipaumbele kwa kila mtanzania na sivyo vinginevyo.
Naye Chifu Wiliam Machimu Mwenyekiti wa Taasisi ya Wafikiriaji Duniani (DAWADU) amewaomba Watanzania kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili waweze kuwabaini watu ambao wamekuwa wakileta taharuki na hofu ya kutoweka amani siku ya upigaji wa kura.
Machimu amesema kuwa jukumu la ulinzi na usalama ni la watanzania wote lakini ni muhimu wakapewa ushirikiano mkubwa ili waweze kuwabaini wale wote wanaotaka kuchafua sifa ya amani iliyokuwapo tokea chaguzi ambazo zimewahi kufanyika
"Hata hivyo tunaamini vyombo vyetu vya ulina na usalama vimejipanga kwa kuhakikisha uchaguzi utakaofanyika Oktoba mwaka huu utakuwa wa amani,utulivu na uhuru na uwazi kinachohitajika ni kila mtanzania kuheshimu maadili tuliyokuwanayo,"amesema Machimu

Post a Comment