‎RC DODOMA AONGOZA MATEMBEZI YA AMANI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

  


‎Na Edward Winchislaus

‎Leo, Oktoba 18, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, ameongoza mazoezi ya kutembea kwa ajili ya kuhamasisha amani, yaliyoanzia lango kuu la Bunge hadi viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma. Zoezi hilo ni sehemu ya kampeni maalum ya mkoa wa Dodoma ya kuhamasisha utunzaji wa amani kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.

‎Matembezi hayo yamehusisha viongozi wa dini, maafisa kutoka vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na wananchi kutoka makundi mbalimbali, yakiwa yamebeba kaulimbiu ya: "Nitalinda amani ya nchi kabla, wakati na baada ya uchaguzi." Kaulimbiu hiyo imesisitiza dhamira ya pamoja ya kudumisha mshikamano na utulivu katika kipindi hiki muhimu kwa Taifa.

‎Akihutubia  wananchi waliokusanyika katika viwanja vya Nyerere Square baada ya matembezi hayo, Mhe. Senyamule amewataka wakazi wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla kuweka mbele uzalendo, mshikamano, na maelewano katika kipindi chote cha uchaguzi.

‎“Jambo hili lilianzia kwenye makundi mbalimbali ambayo nimekuwa nikikutana nayo kusikiliza kero zao. Mwaka huu tumeongeza kipengele cha uchaguzi kwa kuwa tunajua tunalo tukio kubwa la kitaifa. Tulikubaliana kuwa tukutane kama wanajamii tukiwa pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama, ili kila kundi litamke kuwa linataka amani,” alisema Mhe. Senyamule.

‎Aliongeza kuwa“Amani ni kama taa inayowaka gizani. Bila amani, hakuna maendeleo. Nawashukuru wana Dodoma kwa kuihifadhi amani kwa miaka yote. Amani hii haikujitokeza tu kwa bahati; iliasisiwa na waasisi wetu na ni wajibu wetu sote kuilinda na kuienzi.”

‎Aidha, ametoa wito kwa wananchi kujiepusha na lugha za matusi, uchochezi na upotoshaji, hasa kupitia mitandao ya kijamii. Amesisitiza umuhimu wa kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa amani bila hofu, huku akiahidi kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vitashirikiana kwa karibu na wananchi ili kuhakikisha mchakato mzima wa uchaguzi unafanyika kwa ufanisi na kwa kufuata sheria na taratibu.

‎Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Jabir Shekimweri, amewataka viongozi wa dini kuendelea kuwa mabalozi wa amani kupitia nyumba zao za ibada.

‎“Nyumba za ibada ni mahali muhimu pa kukuza maadili na mshikamano. Viongozi wa dini mna nafasi ya kipekee ya kuwaelimisha waumini kuhusu thamani ya amani, hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi,” amesema Mhe. Shekimweri.

‎Hamasa hiyo ni sehemu ya mikakati ya Mkoa wa Dodoma katika kuhakikisha kuwa Uchaguzi Mkuu unafanyika katika mazingira ya utulivu, usalama, na mshikamano, huku wananchi wakihimizwa kushiriki kikamilifu na kwa amani kwa ajili ya mustakabali wa Taifa.

Post a Comment

Previous Post Next Post