MIRADI YA SH BILIONI 23 KUIMARISHA HUDUMA ZA UTALII HIFADHI YA MIKUMI

 Miradi ya Sh Bilioni 23 Kuimarisha Huduma Za Utalii Hifadhi ya Mikumi 


Paskari Ntandu, Askari wa Uhifadhi Daraja la Pili akitoa maelezo juu ya mradi wa upanuzi na uboreshaji wa Uwanja wa ndege wa Kikoboga ulipo kwenye hifadhi ya Taifa ya Mikumi Mkoani Morogoro.

Na Valentine Oforo, Morogoro

HIFADHI ya Taifa ya Mikumi inatekeleza miradi mikubwa miwili ya ujenzi wa miundombinu ya upanuzi wa kiwanja cha Ndege pamoja na nyumba za malazi ili kukidhi mahitaji ya ongezeko kubwa la watalii wa ndani na nje ya nchi.

Miradi hiyo ambayo inatekelezwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 23 ikiwa ni fedha za Benki ya Dunia kupitia mradi wa kuendeleza maliasili na kukuza utalii REGROW huku kukiwa na ushirikishwaji wa Sekta binafsi hususani kwenye eneo la kuwekeza katika huduma za malazi.

Kwa sasa, hifadhi ya Mikumi ambayo ni ya nne kwa ukubwa nchini Tanzania inapokea zaidi ya wageni 1000 kwa siku, ongezeko linaloshuhudia wazawa wengi wakitembelea Hifafi hiyo.

Afisa Muhifadhi Daraja la Pili, Zamzam Yusuph amesema katika kipindi kifupi cha kuanzia Julai 2024 hadi sasa hifadhi imefanikiwa kukusanya Asilimia 89 ya mapato yaliyokadiriwa kukusanywa kwa mwaka huu, ambayo ni zaidi ya Shilingi Bilioni 6.8.

"Rekodi zetu zinaonyesha kuwa jumla ya wageni wapatao 115,009, kutoka ndani na nje ya nchi, walitembelea hifadhi katika kipindi cha kuanzia Julai 2024 hadi Januari 30, 2025, na kutuwezesha kukusanya zaidi ya 6.4bn/ -," alisema.

Kwa upande wake, akizungumzia juu ya mafanikio hayo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Hifadhi ya Taifa ya Mikumi Augustine Massesa kuanza kufanya kazi kwa mradi wa Treni ya Umeme kupitia reli ya kiwango cha Kimataifa SGR kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma kumetoa mchango mkubwa katika ongezeko la watalii wa ndani na nje wanaotembelea hifadhi hiyo inayopatikana mkoa wa Morogoro.

"Kwa sasa, watalii wengi wa ndani, hususani wanawake wanatembelea kwa wingi hifadhi zetu hatua muhimu ya maendeleo inayochochewa na uhakija wa usafiri wa Treni za SGR," alieleza.


Kamishna Massesa alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kukuza sekta ya Utalii nchini Tanzania,  hatua ambayo imeiwezesha hifadhi hiyo kukua kwa kasi.

"Filamu za Tanzania: The Royal Tour na Amazing Tanzania, zimetoa chachu kubwa katika kuhamasisha watalii wengi, wa nje na ndani kutembelea kwa kasi katika hifadhi za Taifa, ikiwemo Mikumu," alisema.

Akifafanua zaidi juu ya utekelezaji wa miradi katika hifadhi hiyo, Paskari Ntandu, Askari wa Uhifadhi Daraja la Pili, alisema miradi hiyo, miongoni mwa mambo mengine inajumuisha ujenzi wa kituo maalamu cha kuwapokea wageni na kutoa taarifa muhimu za hifadhi.

"Kituo kitakuwa na sehemu maalumu ya kupokea wageni, maduka, sehemu ya makumbusho, ukumbi wa maonyesho,  vyoo pamoja na sehemu ya kupaki magari," alisema.


Afisa Muhifadhi Daraja la Pili, Zamzam Yusuph

Kwa upande wa upanuzi na uboreshaji wa uwanja wa ndege wa Kikoboga Airstrip, Ntandu amesema mradi huo unahusisha upanuzi wa barabara za mikimbio ya ndege, ujenzi wa jengo la zima moto na uokoaji,  pamoja na sehmu za maegesho ya ndege.

MWISHO


Post a Comment

Previous Post Next Post