MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inafanya uchunguzi kubaini kilichosababisha kufutika baadhi ya maelezo muhimu kwenye vitambulisho vya Taifa 21,224 vilivyotolewa hivi karibuni na kusambazwa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Julai 21Julai 2024 ,Mkurugenzi wa Idara ya Vitambulisho, Edson Guyai, amesema mamlaka inachunguza ikiwa tatizo hilo limetokana na hitilafu za mashine za uzalishaji, wino au kadi ghafi ili kulitatua bila gharama zaidi.
"Tunawasa wananchi kuchukua hatua wanapokutana na vitambulisho vya namna hii,mtu yeyote ambaye kitambulisho chake kina kasoro kama hizo anapaswa kukirudisha kwenye kituo cha kukusanyia au ofisi ya NIDA iliyopo karibu naye," amesema Guyai.
Ameongeza kuwa mamlaka inatambua kuna vitambulisho 21,224 vyenye kasoro, ikiwa ni pamoja na kufutika majina, picha na tarehe za kuzaliwa.vitambulisho hivyo ni sawa na asilimia 0.09 ya vitambulisho vya taifa 21,322,098 vilivyotolewa.
Aidha amesema kuwa serikali ilitenga Sh. bilioni 42.5 kwa ajili ya kununua kadi za ghafi Oktoba mwaka jana.
Amesema lengo la kupatiwa fedha hizo lilikuwa ni kuboresha uzalishaji wa vitambulisho, usambazaji na utoaji kadi za kitambulisho cha taifa pamoja na kukidhi mahitaji ya umma.
Guyai amesema mchakato huo ulilenga zaidi kutoa kadi za vitambulisho kwa raia wote wenye namba ya utambulisho kwa kuzisambaza kupitia mamlaka za serikali za mitaa na ofisi za NIDA nchini.
Katika hatua nyingine Guyai amesema kuwa Kumekuwa na habari potofu kuhusu ubora wa vitambulisho na kubainisha kuwa vinakidhi viwango vyote vya kimataifa vinavyohitajika.

Post a Comment