Na.Elimu ya Afya Kwa Umma.
Katika kutekeleza Kampeni ya Mtu ni Afya, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Ntuli Kapologwe amesema kitendo cha kufanya mazoezi ya mwili kina msaada mkubwa katika mwili wa binadamu ikiwemo kujikinga na Magonjwa Yasiyoambukiza,kuweka utimamu wa mwili na akili pamoja na kusaidia mmeng’enyo wa chakula.
Dkt. Kapologwe amebainisha hayo Jijini Dar Es Salaam katika Tamasha la Michezo lililokwenda sambamba na Jogging kilometa 8.5 ,utoaji wa elimu ya afya,na uchangiaji wa damu kwa hiari lililoandaliwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Azzah Sports Foundation Idd Azzan.
Mkurugenzi huyo wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya amesema mazoezi ya mwili yana faida lukuki kwa afya ya binadamu hivyo ni wajibu kwa kila mmoja kubadili tabia na kujikita kwenye mazoezi.
" Kitendo cha kufanya mazoezi ya mwili kina msaada mkubwa sana katika kujikinga na magonjwa ya kuambukiza na Yasioambukiza, achalia mbali umuhimu wake katika kuweka utimamu wa mwili na akili Tafiti zinaonesha kuwa mazoezi yanasaidia mmeng'enyo wa chakula, kupunguza uzito uliozidi, kuzuia kuzeeka haraka, kuimarisha ngozi na mifupa, na kuongeza ufanisi wa ubongo”amesema.
Aidha, Dkt. Kapologwe amesema mazoezi yanasaidia kuongeza hamu na nguvu za uzazi, pamoja na kuzuia magonjwa sugu kama vile shinikizo la juu la damu, kisukari, kansa ya ini na mapafu.
“ Ndugu Wananchi, Tunapozungumzia mazoezi, kimsingi tunahimiza aina kuu tatu za mazoezi ambazo ni:- Mazoezi ya kutumia nguvu nyingi kama vile kuinua vitu vizito na push-ups Mazoezi ya kati (aerobics) mfano kufanya Jogging au kuruka kamba Mazoezi laini mfano kunyoosha viungo mbalimbali. Aina zote za mazoezi zina umuhimu wake, lakini sisi Wizara tunasema jambo lolote linalofanya viungo vya mwili kutembea ni sehemu ya mazoezi. Mfano kukimbia, kuruka kamba, kutembea nk. Mazoezi yanaweza kufanyika sehemu yoyote ya wazi ambayo haina vihatarishi mfano mashimo, vitu vyenye ncha kali au shughuli zozote hatarishi za kibinadamu”amesisitiza.



Post a Comment