TANGA YAJIPANGA KUFUFUA UCHUMI WA VIWANDA KUPITIA UWEKEZAJI ELIMU YA UBUNIFU

 

 Na VALENTINE OFORO, Tanga 

SERIKALI mkoani Tanga inatekeleza mkakati kabambe wa kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi ili kuwekeza katika fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana katika mkoa huo uliopo kaskazini-mashariki mwa Tanzania. 



Miongoni mwa wawekezaji wanaokusudiwa na mkakati huo ni wale wa sekta ya elimu, ubunifu na teknolojia, hususani katika usindikaji wa mazao na uongezaji thamani.

Licha ya kuwa na hali ya hewa nzuri ya kusaidia uzalishaji wa matunda, viungo na mazao mengine maarufu ya biashara na chakula, kukosekana kwa viwanda vya usindikaji kumetajwa kusababisha mkoa kutonufaika ipasavyo.

Pamoja na changamoto hiyo, imeelezwa kuwa watumishi wengi wa umma, na wale kutoka sekta wa kibinafsi wanashindwa kujiendeza kielimu kupitia programu maalumu zinatolewa na vyuo vikuu mbalimbali kwa sababu hakuna chuo kikuu chochote katika mkoa wa Tanga.

Akiongea na waandishi wa habari mapema leo (Jumapili, May 26, 2024) kuhusu maandalizi ya maazimio ya kitaifa ya mwaka huu ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2024, Mkuu wa Wilaya ya Tanga mjini, Mhe. James Kaji amesema Serikali mkoani Tanga imeazimia kutekeleza programu mbalimbali za kuchochea sekta za teknolojia, ujuzi, ubunifu na ujasiriamali ili kufufua uchumi wa viwanda.

"Sisi Tanga, tunashukuru sana Serikali ya awamu wa sita inayoongozwa na Mhe Dr Samia Suluhu Hassan kwa kutupa fursa ya kuwa wenyeji wa wiki hii muhimu," 

"Hatua hii ni muhimu sana kwetu kwani itasaidia sana kuchochea kasi ya jitihada zetu za kufufua viwanda," alisema.



Mhe. Kaji aliwataka wakulima, wajasiriamali wadogo na wakati, wanafunzi na wananchi wote wa Tanga na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi ili kupata fursa adhimu ya kujifunza teknolojia mbalimbali za kibunifu.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda anatarajia kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa maonyesho hayo muhimu yanayofanyika kwa muda wa wiki moja katika viwanja vya shule ya Sekondari ya Popatilal iliyopo jijjni Tanga. 

Zaidi ya Taasisi 300 zinashiriki maonyesho hayo, ikiwa ni pamoja na Vyuo Vikuu, Vyuo vya kati, Wizara, Taasisi zs Kimataifa, Taasisi za Tafiti za Kilimo na Mifugo, pamoja ms wabunifu katika sekta mbambali.


Post a Comment

Previous Post Next Post