MAVUNDE AJA NA MKAKATI KABAMBE KUWAWEZESHA WANA DODOMA KIUCHUMI

 

Na VALENTINE OFORO 

MBUNGE wa Dodoma mjini ambaye pia ni Waziri wa Madini, Mh.Anthony Mavunde amesema kuwa Jimbo lake la Dodoma mjini litakua linatenga Sh milioni 20 kila mwaka kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.



Fedha hizo, amesema zitakuwa zikitumika kwa ajili ya kugharamikia manunuzi ya mashine na mitambo midogo ya kuzalisha bidhaa, na kuongeza thamani ya bidhaa na malighafi mbalimbali zinazozalishwa mkoani Dodoma, na nchi nzima kwa ujumla.



Mhe Mavunde ameyasema hayo katika hotuba yake fupi ya kuzindua rasmi  mafunzo ya ujasiriamali yaliyoratibiwa na Jeshi la Polisi pamoja  na Kanisa Halisi la Mungu Baba, Jijini Dodoma. 

“Kutokana na nia ya dhati ya Rais wetu mpendwa Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan  ya kuwainua wananchi kiuchumi amerejesha tena ile mikopo ya asilimia 10 isiyo na riba na hii itawasaidia kuondokana na mikopo kausha damu;"

"Ili mkopo huo ulete tija,ni lazima tuwaandae wana Dodoma kupata mafunzo ya ujasiriamali na ujuzi mbalimbali wa uzalishaji bidhaa kupitia mafunzo kama haya ya leo,"


"Kwangu kama Mbunge nimekuja na progamu ya kukiinua kikundi kimoja kila mwaka kwa kutoa Tsh 20,000,000 ya ununuzi wa mashine na mitambo kuanzisha viwanda vidogo vidogo”alisema Mavunde



Kwa upande wake, kiongozi Mkuu wa Kanisa Halisi la Mungu, Baba Halisi, ameishukuru Serikali na viongozi wote wa mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na kanisa hilo  kwa karibu,  na kueleza dhumuni la mafunzo hayo ya siku nne ni kuiandaa jamii kushiriki kikamilifu katika uchumi wa Taifa.

"Moja kati ya majukumu makubwa ya huduma za kanisa hili ni kuwafundisha waumini wake, na watanzania wote kwa ujumla namna ya kuzalisha mali kwa njia za haki na siyo dhuluma," Baba Halisi alisema.

Pamoja na hayo, Baba Halisi amewataka watanzania kufanya kazi kwa bidii ili kujenga uchumi wa nchi, na wa mtanzania mmoja mmoja, kwani ibada halisi anayoitaka Mungu ni uzalishaji mali.

"Kwetu sisi, ibada siyo kukusanyika kanisani na kuomba tu, bali ibada ni kila kitu ambacho mtu anafanya kwa haki, yaani kumtanguliza Mungu na kujiepusha na udanganyifu na dhuluma," alisisitiza .



Hapo awali akimwakilisha Afande RPC Mkoa wa Dodoma Afisa Polisi Jamii Mkoa wa Dodoma, Afande Eva Michael Stesheni, ameipongeza Kanisa Halisi la Mungu Baba kwa kuja na wazo hilo la kuwainua wananchi kiuchumi kwani linaenda sambamba na mipango iliyopo katika Jiji la Dodoma.

"Kupitia mafunzo haya idadi kubwa ya wanajamii itapata ujuzi wa kushiriki katika uzalishaji mali na hivyo kupunguza vitendo vya uhalifu katika jamii.



Post a Comment

Previous Post Next Post