WAZIRI NDUMBARO AAGIZA MKANDARASI UWANJA WA ARUSHA KUTOA AJIRA KWA WAZAWA.

 


Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe Dkt. Damas Ndumbaro amemuagiza Mkandarasi anayejenga Uwanja wa Mpira wa Miguu Jijini Arusha, Kampuni ya China Railway Construction Engineering Group ( CRCEG) kutoka China ahakikishe kuwa  anatoa ajira kwa wazawa wa Mkoa huo.



Mhe. Ndumbaro ametoa maelekezo hayo wakati wa hafla ya kumkabidhi Mkandarasi huyo eneo la ujenzi wa uwanja wa Arusha lililopo Kata ya Olmoti tarehe 6 Aprili 2024, ambapo amesema ujenzi huo utakamilika mapema mwaka 2026.


Amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amekubali Uwanja huo ujengwe Jijini Arusha na kuridhia kiasi cha Shilingi Bilioni 286 kitumike kukamilisha kazi hiyo.


"Ujenzi huu ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 ambayo inaelekeza ujenzi na ukarabati wa miondombinu ya Michezo kwa manufaa ya wananchi, lakini pia ni maandalizi ya michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) mwaka 2027" amesema Mhe. Ndumbaro.



Kwa upande wake Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Slaa amesema kuwa Wizara yake  italipima eneo hilo na kuweka mipaka , ambapo pia ameagiza Watendaji wa Idara ya Ardhi wahakikishe wanatekeleza maelekezo hayo ndani ya siku tisini.


Naye, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo Mhe. Mussa Sima amemsisitiza  Mkandarasi ahakikishe mradi huo unakamilika kwa wakati, ukiwa na viwango vinavyotarajiwa na kuwa na usimamizi na ufuatiliaji wa mara kwa mara.



Awali Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Gerson  Msigwa amesema  uwanja huo utakua na uwezo wa kubeba watazamaji 30,000 na unajengwa katika eneo lenye ukubwa wa ekari 36  ambapo eneo lingine lenye ukubwa wa ekari 44.1 litatumika katika awamu ya pili na tatu kujenga miundombinu mingine ya michezo.




Uwanja huo ukikamilika utaongeza idadi ya viwanja vitakavyotumika katika mashindano ya AFCON pamoja na uwanja wa Benjamin Mkapa na Aman Zanzibar.

Post a Comment

Previous Post Next Post