CHAMWINO YAFURAHIA UTEKELEZAJI MRADI WA LTIP

 

Na. Magreth Lyimo, MLHHSD


Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) imejikita katika kutoa elimu ya masuala ya ardhi katika Wilaya ya Chamwino Mkoa wa Dodoma ambapo takribani mipango ya matumizi ya ardhi 63 imeandaliwa kutokana na ushirikishwaji mzuri unaofanyika wilayani humo.



Hayo yamesemwa na msimamizi mradi katika Wilaya ya Chamwino Bi. Grace Mbena tarehe 7 Aprili 2024 katika bonanza la kuwahamasisha wanachi kushiriki zoezi la umilikishwaji lililofanyika katika viwanja vya michezo vya kijiji   cha Iringa Mvumi zamani ambalo lililandaliwa na timu ya mradi Wilayani humo mkoani Dodoma.


"Bonanza hili limejumuisha vijiji vitatu kutoka katika Wilaya ya Chamwino ambavyo ni Iringa mvumi zamani, Iringa mvumi na Cheta ambapo wananchi walicheza michezo mbalimbali kama mpira wa miguu, kuvuta kamba, ngoma" alisema Mbena



Aliendelea kusema kuwa zoezi hili litaendelea katika vijiji vilivyobakia kwa kuwa lengo ni kuwa na mipango ya matumizi ya ardhi 80, kuboresha mahusiano kati ya timu ya utekelezaji mradi pamoja na wananchi wa wilaya hiyo ili kutekeleza kazi hizo kwa pamoja.


Msimamizi wa masuala ya kijamii na kimazingira wa mradi Bw. Alpha Mangula alisisitiza kuwa lengo kuu la kuandaa bonanza hilo ni kutoa elimu juu ya umilikishwaji na utoaji wa hati miliki za haki miliki za kimila, haki za umiliki wa ardhi kwa wanawake na makundi mengine maalumu kama wazee, walemavu, vijana na watoto aidha wananchi kutambua umuhimu wa kushiriki vikao vya uhamasishaji na kuwepo maeneo yao wakati wa utambuzi wa vipande vya ardhi .



Nae mwananchi kutoka kijiji cha Iringa Mvumi mpya Bw. Said Sulemani amesema kuwa bonanza hili limewaleta wananchi pamoja na kuahidi kutoa ushirikiano kwa wataalamu.


Mradi huu unatekelezwa chini ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ukiwa na lengo kuu la kuboresha usalama wa milki za ardhi kwa kuzingatia masuala ya kijamii na kimazingira ambapo kwa upande wa vijijini mradi utatoa takribani hatimiliki za hakimilki za kimila 500,000 pamoja na vijiji 1667 kuandaliwa mpango wa matumizi ya ardhi.




Post a Comment

Previous Post Next Post