Na Paul Kayanda, Kahama
KATIKA kuelekea Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani, Mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Shinyanga, Christina Mzava amewataka Wazazi na walezi Mkoani humo kuwajibika Ipasavyo katika malezi ya Watoto wao kuwapatia haki yao ya msingi kuwafuatilia nyenendo zao pindi wanapokuwa shuleni ikiwemo kuwapatia mahitaji yao ya lazima ya kila siku na siyo kuwaachia walimu peke yao.
Pia Mbunge huyo amekemea tabia ya wanawake kuwafanyia ukatili watoto ambao hawajawazaa kwani mtoto hana kosa, aliletwa na baba ama aliachwa na mama yake, hali inayosababisha ongezeko la watoto wa mitaani kutokana na manyanyaso ya mama wa kambo.
“Mama unaondoka unaacha watoto wako, beba ondoka nao huo ni msalaba wako kwa sababu hujui huku nyuma baba ataoa mwanamke wa aina gani au baba unaondoka unaacha watoto wako hujui mamaataleta baba wa aina gani kwa mana hiyo hata wanaume wananyanyasa watoto wao wa kambo ndiyo hali inayopelekea baba kulawiti watoto wake na mama anachoma watoto moto,” amesema Christina Mzava Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Shinyanga.
Mzava amesema hayo alipokuwa akizungumza na Waaandishi wa Habari mara baada ya kutembelea shule ya msingi Nyashimbi ambako amewaongoza Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi CCM (UWT) Kata ya Mhongolo kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani ambapo wamefika shuleni hapo kwa lengo la kutoa msaada wa Madaftari, Kalamu pamoja na Taulo za kike.
Pamoja na Mambo mengine pia mbunge huyo ameguswa na uhaba wa madawati katika shule hiyo kutokana na upungufu wa madawati 500 ambapo kama Mbunge ameahidi kuchangia madawati 20 yenye thamani ya shilingi Mil. 1.6 huku akiahidi kumleta Mbunge mwenzake wa Jimbo la Kahama Mjini Mhe. Jumanne Kishimba ili naye atoe mchango wake hali ambayo itapelekea kupunguza uhaba huo.
Hata hivyo Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Mtelemla John Mandalu amemweleza mbunge huyo kwamba shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa Vyumba vya madarasa manne hali ambayo inapelekea Wanafunzi kusoma kwa zamu kwamba wengine wanaingia asubuhi na wengine wanaingia mchana na kuongeza kuwa kuna vyumba vingine havina hata dawati moja.
“Kubwa kabisa linalotukabili hapa ni upungufu wa madawati pamoja na upungufu wa vyumba vya madarasa kwa upande wa madawati tunaupungufu wa madawati 300 ambapo jumla ya Wanafunzi waliopo shuleni hapa ni 1800, na ninayo madarasa mawili hayana madawati kabisa, kwamba ili wanafunzi waweze kukaa inavyotakiwa tunahitaji vyumba vinne vya madarasa,” amesema Mwalimu Mkuu.
Katika hatua nyingine Mbunge wa Viti maalumu Christina Mzava ameguswa na familia ya Mzee Mabala Masalanganya na kumkabidhi fedha kiasi cha shilingi Elfu 50 na kumwahidi Neti pamoja na Blanketi zito kutokana na kipindi hili ni msimu wa mvua za masika na baridi na kuongeza kuwa hataishia hapo katika kusaidia vikongwe hao ambao hawana watoto wala mtu wa kuwaangalia.
Wakati huohuo UWT nao wameweza kumpatia msaada wa Unga wa sembe zaidi ya kilo 10 pamoja na sabuni kwaajili ya kuwasaidia kufua nguo na chakula huku Mzee Mabala akimshukuru Mbunge huyo pamoja na UWT kwa msaada wao kwani hakuna mtu ambaye amewahi kufika nymbani kwake kwaajili ya kutoa msaada kama huo jambo ambalo limegusa mioyo yao.
“Mimi kama mwakilishi wa familia nashukuru sana kwa msaada wenu hapa najua nimepona hata kunguni wananing’ata kila kukicha naogopa hata kukaribisha watu ndani kwani wanaweza kunikimbia kwa maana kunguni ni hatari sana na wanafedhehesha,” alilalamika Mzee Mabala Mkazi wa Nyashimbi.


.png)

Post a Comment