UKAGUZI WA VYANZO VYA MIONZI WAENDELEA NCHINI

 Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) inaendelea na zoezi la ukaguzi wa vituo vinavyotumia mionzi nchini ili kuhakikisha matumizi ni salama  kwa wafanyakazi wa vyanzo vya  mionzi, wananchi pamoja na mazingira.



Akizungumza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita baada ya kufanya zoezi la ukaguzi, Mkaguzi Mwandamizi wa mionzi wa TAEC Bwn. JEROME MWIMANZI amesema ukaguzi huo ni muhimu ili kujiridhisha kama mashine zinafanya kazi vizuri, majengo hayavujishi mionzi  sambamba na watumiaji kufuata sheria, kanuni na taratibu za matumizi salama ya mionzi.


Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita Dkt. MFAUME SALIM KIBWANA amesema anaishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. SAMIA SULUHU HASSAN kwa uwekezaji mkubwa wa mashine za uchunguzi kwa kutumia mionzi katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Geita.


Naye Mtekinolojia wa mionzi  katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Geita YOHANA SOSPETER amesema ukaguzi wa TAEC unawasaidia katika kuhakikisha utoaji wa huduma ya mionzi inakuwa salama kwa wagonjwa wanaowahudumia pamoja na kujilinda wao kama watoa huduma dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mionzi.



Katika ukaguzi uliofanyika Mkoani Mwanza jumla ya vituo 48 vimekaguliwa zikiwemo hospitali, viwanda, uwanja  wa ndege, ujenzi wa reli ya SGR Pamoja na Daraja la kigongo busisi ambapo kati ya hivyo vituo vinne vimefungiwa kutoa huduma hadi hapo vitakapo kidhi matakwa ya sheria na kanuni za kumiliki na kutumia vyanzo vya mionzi.

Post a Comment

Previous Post Next Post