Waziri wa Habari Teknolojia ya Habari na Mwasiliano, Nape Nnauye amesema ameuona mjadala unaoendelea baada ya TCRA kusema itawachukulia hatua baadhi ya Watangazaji wanaosoma magazeti kwa mbwembwe huku wakiongezea baadhi ya vitu visivyotakiwa wakati wa usomaji ambapo Waziri Nape amesema ameelekeza TCRA kuruhusu ubunifu kwenye tasinia ya habari.
Kwenye andiko lake kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter) Nape ameandika “Nimeuona mjadala wa “kusoma magazeti” , nimeelekeza TCRA kuruhusu ubunifu kwenye tasnia ya habari, staili ya usomaji we magazeti imeongeza mvuto kwenye usomaji huo, ni jambo linapaswa kutiwa moyo badala ya kuzuiwa, Waandishi endeleeni na ubunifu kwenye kusoma magazeti”
“Maelekezo mengine yeyote ambayo TCRA inatoa kwenye sekta ya habari yanapaswa kuwa wezeshi na sio zuizi, ni muhimu TCRA ijenge utamaduni wa kuzungumza kabla ya kuagiza”
Itakumbukwa jana Meneja wa Huduma za Utangazaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Andrew Kisaka, wakati akiongea katika mkutano wa mwaka wa Vyombo vya Utangazaji Nchini uliofanyika Jijini Dodoma alinukuliwa akisema “Kuna wachache wakorofikorofi wanaleta mbwembwe na kuongezea vitu pale kwenye magazeti kwahiyo nafikiri hao pia watamulikwa na kushughulikiwa kwa mujibu wa kanuni na sheria, ni wachache sana”

Post a Comment